November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasichana vinara waiomba serikali kuondoa kodi kwenye taulo za kike

Na Mwandishi wetu Timesmajira online

WASICHANA vinara 50 wanaotoka ndani na nje ya mfumo rasmi wa elimu kutoka katika mikoa mitano wameiomba Serikali kuondoa kodi katika bidhaa za taulo za kike ‘pedi’ ili kuonesha nia njema ya kuheshimu na kutambua mchango wa wasichana na wanawake katika taifa.

Pia wameiomba Serikali kuweka kipaumbele katika kutenga bajeti ambayo itasaidia kugawa pedi bure kwa wanafunxi wa kike, ili kuwasaidia kusoma kwa uhuru na kupunguza utoro na kuongeza ufaulu kwa wasichana.

Ombi hilo wamelitoa jijini Dar- es- salaam Mei 17,2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya wasichana ya Pedi bure, Pedi bila Kodi ambayo ipo chini ya Shirika la Msichana Initiative na Shirika la Wanawake wa Kifugaji (PWC).

Akizungumza kwa niaba ya wasichana hao Elizabeth Mollel ambaye ni mwanafunzi kutoka shule ya sekondari ya Emanyata iliyopo Loliondo mkoani Arusha amesema hedhi salama bado ni changamoto kubwa kwa wasichana na wanawake wengi Tanzania.

“Sisi wasichana vinara tunaamini kwamba hedhi ni tunu,hedhi ni mwanzo wa maisha ya mwanadamu hivyo ni suala ambalo linapaswa kupewa kipaumbele kwa ustawi wa wasichana na taifa letu kwa ujumla,”amesema.

Amesema mara nyingi msichana anapokuwa katika hedhi huitaji kuanzia pakti mbili na zaidi ili kukamilisha mzunguko wake wa hedhi wa mwezi mmoja.

Ameeleza kuwa kutokana na gharama za taulo za kike kuwa kubwa wasichana wengi wamekuwa wakiishi katika kutumia vifaa visivyorafiki kama vile, vipande vya nguo, majani ya miti na vifaa vingine ambavyo si salama kwa afya zao.

Akitolea mfano amesema pakiti 1 ya pedi imekuwa ikiuzwa kwa shilingi 2000, na kueleza kuwa bei hiyo inaweza kuwa juu zaidi kulingana na kampuni na mahali inapouzwa.

“Ukiangalia gharama hii ni kubwa sana, hasa kwa wasichana wanaotoka katika kaya maskini ambazo taulo za kike si kipaumbele katika bajeti ya familia,”amesema Mollel.

Vilevile amesema pamoja na kuwepo kwa upatikanaji wa pedi za kufua zinazoweza kutumika zaidi ya mara moja, bado utunzaji na utumiaji wake unaweza kuwa changamoto hasa katika maeneo ya vijijini yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.

Wizara husika iweke bidhaa za pedi kwenye orodha ya bidhaa muhimu, ili kupunguza gharama za uzalishaji na kupunguza bei ya pedi.

Pia aliwasihi wadau wa haki za wasichana kuendelee kutoa elimu kuhusu masuala ya hedhi salama na umuhimu wa elimu ili kuendelea kubadilisha maisha ya wasichana na jamii ya kitanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amesema kampeni hiyo itatekelezwa na wasichana hao vinara inalenga kuangazia umuhimu wa hedhi salama na kuongeza uelewa kwa jamii pamoja na kutambua changamoto wanazokutana nazo wasichana na wanawake ikiwa mazingira hayatakuwa rafiki ili kuzitafutia ufumbuzi.

“Kampeni hii inalenga kuonesha umuhimu na uharaka wa serikali na wadau mbalimbali kutengeneza mazingira wezeshi kwa wasichana na wanawake kupata bidhaa za kujihifadhi wakati wa hedhi,”amesema Gyumi.

Aidha amesema kampeni hiyo ni ya mwaka mmoja na itatekelezwa katika Mkoa wa Dar es salaam, Arusha,Dodoma,Pwani pamoja na Tabora.

Awali Ofisa Mradi kutoka Shirika la Wanawake wa Kifugaji (PWC ), Nang’ambo Mollel amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha inatoa elimu kwa jamii ili iweze kutambua kuwa hedhi salama kwa mtoto wa kike ni sehemu ya afya yake pia ni haki yake.

“Tuhakikisha sauti za wasichana vinara zinaendelea kusikikika sehemu mbalimbali Kwa wadau ili kuhakikisha kwamba ndoto zao zinafanikiwa ikiwemo Pedi kutolewa bure na tozo kuondolewa,”amesema.