March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washukiwa mauaji ya mwanafunzi Mzumbe wauwa,Polisi waeleza walivyowanasa

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limewaua watu watatu wanadaiwa kuwa ni washukiwa wa mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Mbeya,Shyrose Michael Mabula (21), aliyetekwa na kuuawa kikatili mapema mwezi huu.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Septemba 29,2025,Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,Benjamin Kuzaga amesema Septemba 14,2025 iliripotiwa kutekwa kwa nyara kwa mwanafunzi wa chuo kikuu Mzumbe ndaki ya Mbeya aitwaye Shyrose Mabula ambaye alitekwa na watu wasiofahamika.

Kuzaga amesema kuwa Septemba 16,2025 Majira ya saa 5:00 usiku katika mtaa wa  Morovian uliopo kata ya Isyesye mkoani Mbeya mwili wa mwananzi huyo ulikutwa ukiwa umechomwa moto.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza ufuatiliaji ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika katika tukio hilo Septemba 24,2025.

Kamanda Kuzaga amesema kuwa Septemba 24, 2025 saa 4:00 asubuhi alikamatwa ,Marwa Nyahgea John (25)mkazi wa Uzunguni ‘A’ Mbeya ambaye katika mahojiano alikiri kuwa yeye pamoja na wenzake waliohusika na tukio hilo la utekaji na mauaji kwa kushirikiana na Edward Christopher Kayuni, pamoja na Websta William Mwantebele.

Watu hao walivyokamatwa walisema kuwa walimteka nyara Shyrose kwa lengo la kujipatia fedha nyingi kutoka kwa baba yake mzazi, aitwaye Dkt.Mabula Michael.

Baada ya kumteka, walianza kupiga simu kwa familia yake kwa lengo la kujipatia fedha, lakini waliposhindwa kupata walihofia kukamatwa, wakaamua kumuua binti huyo ili kuficha ushahidi.

Aidha ilielezwa kuwa watu hao walijaribu kumpa sumu (dawa ya kuulia magugu Round Up) na baada ya kushindikana walimnyonga kwa kamba na kisha kuchoma mwili wake moto.

Baada ya taarifa hizo, ufuatiliaji uliendelea. Septemba 25, 2025, alikamatwa ,Websta William Mwantebele (27) mlinzi, naye alikiri kushiriki katika tukio la utekaji na mauaji.

Aliwaelekeza polisi sehemu waliyopanga kwenda kuficha miili ya wengine.

Hata hivyo Kamanda amesema kuwa Septemba 27, 2025 askari walikwenda Kijiji cha Chalangwa wilaya ya Chunya ambapo walikuwa wamemwekea mtego mtuhumiwa Websta  Mwantebele.

Akielezea zaidi Kuzaga amesema mtuhumiwa alipogundua anatiwa mbaroni, alijaribu kukimbia huku akirusha visu na askari walifyatua risasi, zikampiga mguuni na mgongoni na kupelekwa hospitali ya Wilaya ya Chunya pamoja na mwenzake lakini wote walifariki .

Aidha, mtuhumiwa Marwa Nyahgea John alionyesha sehemu aliyompeleka Shyrose alipokuwa akiteswa, ambapo alilazimishwa kumpigia baba yake simu na kudai fedha na  baada ya mauaji, vidole vyake vilikatwa na kupelekwa kwa mganga wa jadi kwa ajili ya kufanyia zindiko.

Katika harakati hizo, mtuhumiwa Marwa Nyahgea John alijirusha kutoka kwenye gari la polisi akiwa anapelekwa kuonyesha maeneo mengine na kupata jeraha baya kichwani. alifariki dunia akiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

“Lakini Katika upekuzi waliofanya polisi kwa watuhumiwa hao walikutwa na pingu mbili, vitambulisho bandia vya JWTZ, na simu mbili zilizokuwa na ushahidi wa mawasiliano kuhusu utekaji.

Hata hivyo Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ametoa kwa jamii, hasa vijana waliopata mafunzo mbalimbali ya kijeshi na usalama, kutumia mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria na siyo kwa uhalifu.

Wananchi wanashauriwa kuacha tamaa ya kujipatia mali kwa njia haramu, badala yake wafanye kazi halali kwa ajili ya kipato.

Polisi wanakumbusha kuwa uhalifu hauna nafasi katika jamii, na mkono wa sheria utawafikia wahalifu popote walipo.