January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washtakiwa uhujumu uchumi kwa kujiunganishia umeme kinyemela

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, DSM

WAFANYABIASHARA wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mbele ya mahakimu wawili tofauti wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi kwa kuingilia miundombinu ya TANESCO na kujiunganishia umeme kinyume na utaratibu.

Washitakiwa hao ni Ahmed Khalifa, mkazi wa Mikocheni, Abdulrazak Said na Anuary Amdani, ambao wote ni wakazi wa Temeke na Joseph Mwakabanga, mkazi wa Tandale kwa Tumbo,

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Kassian Matembele, upande wa mashitaka ulidai mnamo Julai 29, 2020 Mikocheni, Mtaa wa Ndovu Wilayani Kinondoni, washtakiwa kwa pamoja, Khalfan na Said waliingilia kwa makusudi miundombinu ya TANESCO.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujiunganisha umeme kupitia mfumo wa TANESCO na kukwepa kutumia mita, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Aidha, mnamo Agosti 7, 2020 katika Mtaa wa Magomeni Mikumi Wilayani Kinondoni jijini Dar es salaam, Amdani na Mwakabanga waliingilia kwa makusudi na kinyume cha sheria miundombinu ya TANESCO iliyokusudiwa kutumiwa kusambaza huduma ya umeme.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa washitakiwa hao walibadilisha mita, mali ya TANESCO kutoka kwenye nyumba inayomilikiwa na Amdani yenye deni ya shilingi 3,521,587.70 na kuweka mita mpya kwa lengo la kukwepa deni lililotajwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu mashitaka yao kwa vile mashiataka yao yanaangukia kwenye sheria ya uhujumu uchumi.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na Mawakili Waandamizi wa Serikali Mantenus Marandu and Wankyo Simon pamoja na Wakili wa Serikali Benson Mwaitenda umedai upelelezi wa mashauri yote mawili haujakamilika.

Baada ya kusomewa mashitaka yao, Mahakimu katika kesi zote mbili walitoa dhamana kwa washitakiwa kwa kuzingatia masharti mbalimbali.

Khalfan na Said walipewa masharti ya kupata wadhamani wawili kila mmoja ambaye angeweka dhamana ya shilingi milioni 5 na Kila mdhamini alitakiwa awe na barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri wake, kuwasilisha vitambulisho vyao, ambayo ni, kadi ya kitambulisho cha Taifa au Kadi ya kupigia kura.

Washtakiwa pia walizuiliwa kuondoka nchini bila kupata ruhusa ya Mahakama.

Kwa upande wa Amdani na Mwakabanga, hakimu aliwapa dhamana kwa masharti ya kupata wadhamini wawili kila mmoja ambaye atasaini dhamana ya 500,000 / na walitakiwa kuwasilisha vitambulisho vyao.

Kesi zote ziliahirishwa hadi Septemba 10, 2020.