September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washtakiwa saba,mauaji ya Lucas wapandishwa kizimbani

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Kagera


Kesi inayowakabili washtakiwa 7 wa mauaji ya Baraka Lucas ( 20 )akiwemo Mkuu wa kituo cha Polisi Kisiwa cha Goziba ( OCS )John Mweji,wamefikishwa kwa mara ya pili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Janeth Masese kwa mara ya pili.

Ambapo wakili wa Serikali Agness Owino amesema shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa huku akiiomba Mahakama hiyo kutaja tarehe nyingine kwa sababu upelelezi wa kesi hiyo namba 18914 ya mwaka 2024 haujakamilika.

Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Wakili wa Serikali Agness Owino,amesema shauri la uchunguzi limefikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa ambapo washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kukamilisha taratibu za upelelezi.

Owino,amewataja washtakiwa hao kuwa ni John Mweji, ambaye ni mshitakiwa wa kwanza ,Ahmad Rashid ,Francis Patrick,Ally Jumanne Ally,Emmanuel Mafuru Massatu ,Evodius Benedictor Rukaka na Athuman Seleman Malindo.

Kwa upande wa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera Janeth Masese ,amesema shauri hilo litatajwa tena Agosti 06 mwaka huu majira saa 4.30 asubuhi na washitakiwa wote wamerejeshwa rumande.

kesi hiyo ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 09 mwaka huu.

Ambapo Juni 15 mwaka huu Jeshi la polisi lilitoa taarifa ya kuuawa kwa Baraka Lucas na kudai kuwa wanafanya uchunguzi wa kubaini chanzo cha kifo na watuhumiwa waliohusika katika mauaji hayo.

Taarifa kutoka kwa wananchi zinasema marehamu alikamatwa na polisi Juni 9 mwaka huu na Juni 12 mwili wake ulionekana kando kando ya ziwa Victoria akiwa amekufa huko kisiwani Goziba.

Kati ya washtakiwa 7 wa mauaji hayo 4 ni askari polisi na mgambo 3.