December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washitakiwa tisa mauaji ya mtoto Asimwe,wapandishwa kizimbani kwa mara ya pili

Na Ashura Jumapili, Timesmajira Online Kagera

KESI inayowakabili washtakiwa tisa wa mauji ya mtoto Noela Asimwe Novart (2.5) aliyekuwa mwenye ualbino wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera Elipokea Yona kwa mara ya pili ambapo Wakili wa Serikali Erick Mabagala amesema shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa.

Mabagala, ameiomba Mahakama hiyo kutaja tarehe nyingine wakati wakiendelea na mchakato wa kusajili kesi hiyo Mahakama Kuu ambayo ni namba 17740 ya mwaka 2024.

Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Wakili wa Serikali Erick Mabagala, amesema shauri la uchunguzi limefikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa ambapo washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili wa shauri kupelekwa Mahakama Kuu.

Mabagala,amewataja washtakiwa hao kuwa ni Elipidius Rwegoshora ambaye ni mshitakiwa namba moja ,Novart Venant,Nurdin Masud,Ramadhani Selestine,Rwenyagira Alfonce,Dastan Buchard,Faswiu Athuman,Gozbart Arikad na Dezideri Everigist.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Elipokea Yona, amesema shauri hilo litatajwa tena Julai 26 mwaka huu ambapo mshitakiwa namba moja Elipidius Rwegoshora amepata Wakili wa utetezi Mathias Rweyemamu, ambapo ameahirisha kesi na washitakiwa wamerejeshwa rumande.