January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washiriki zaidi ya 2000,kushiriki TRA Marathon

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

Zaidi ya watu 2000, wanatarajiwa kushiriki katika mbio za TRA (TRA Marathon) katika wiki ya EFD inayotarajiwa kuanza Septemba 23 mwaka huu huku wito ikitokea kwa wengine kuendelea kujisajili zaidi ili waweze kushiriki.

Mbio hizo zilizoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zitaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam, ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kusindikizwa na kauli mbiu ya ” Risiti Yako ni Ulinzi Wako”,zitaambatana na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu na mbio za magunia kwa siku tofauti.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Septemba 20, mwaka huu MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema mbio hizo zitakuwa za kilometa 5 na kilometa 10 huku akitoa idadi ya watu waliojisajili kushiriki mbio hizo kuwa ni watu 600 huku idadi inayotarajiwa kuwa ni ya watu zaidi ya 2000.

Mpogolo amesema kuwa, lengo la mbio hizo ni kuhamasisha matumizi sahihi ya Mashine za Risiti za Kielekroniki (EFD) na utoaji wa risiti, kujenga uhusiano baina ya wafanyabiashara na Maofisa wa TRA pamoja na kujenga afya kupitia michezo.

Mbio hizo zitaanzia uwanja wa Jakaya Kikwete, kilichopo Mnazi Mmoja Kidongo Chekundu, ambazo zitaanza saa 12 alfajiri na kutarajiwa kumalizika saa 2 asubuhi.