November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasanii watakiwa kuacha Kiki, kutumia bure Akaunti zao binafsi YouTube

Na Grace Semfuko, TimesMajira Online

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara yake, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wamekubaliana kubadilisha Kanuni ili wasanii na wadau wengine wa maudhui yasiyohusisha uchakataji wa habari waweze kurusha kazi zao kwenye akaunti zao binafsi za YouTube bila kufanya usajili na malipo kwa TCRA.

Akizungumza na Viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) na vyama vinavyounda shirikisho hilo Jijini Dar es Salaam, Dkt. Abbasi amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kuona umuhimu wa kuwanufaisha Wasanii na kukuza Sanaa nchini.

“Tumefanya mazungumzo na wenzetu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na TCRA kuhusu maudhui ya Tv za mtandaoni, tumeona kuna tofauti kubwa sana kati ya Habari na Sanaa, hivyo tutaboresha kanuni, tumeona eneo hili la Wasanii linapaswa kufanya kazi zao bure, sasa nafurahi kuwaambia kuwa kuanzia sasa wasanii wawe wa muziki au filamu changamoto hii imefika mwisho,” amesema Dkt Abbasi.

Akizungumzia Kuhusu maslahi ya kazi za Wasanii zinazorushwa kupitia vyombo mbali mbali vya habari, Dkt. Abbasi amesema, Wizara yake kupitia taasisi zinazosimamia Wasanii ikishirikiana na TCRA wanaendelea kupitia na kuanzisha mfumo wa kuangalia namna ya kazi zao zinavyorushwa kwenye vyombo hivyo ili waweze kulipwa kwa jinsi zinavyorushwa.

Aidha aliwataka Wasanii kutumia maeneo na mazingira ya uhalisia wakati wa kurekodi kazi zao ikiwa ni pamoja na kutangaza miradi ya ajenda za kitaifa lengo likiwa ni kutafuta fursa za wageni kutembelea maeneo hayo ili kukuza uchumi wa taifa kupitia utalii.

“Tuna miradi mikubwa tunaifanya hapa nchini na kwenye hifadhi zetu za wanyama na kwingineko mnakodhani ni vizuri mkatangaza, tumieni “location” kama zile kutangaza fursa za utalii katika nchi yetu,” amesema.

Hata hivyo, Dkt. Abbasi amewataka Wasanii ‘kuacha kiki’ na kutumia taaluma zao vizuri katika kutangaza kazi zao badala ya kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii na kueleza kuwa kwa kufanya hivyo wanaondoa uaminifu kwa jamii ambao wameujenga kwa gharama kubwa.

“Wote mmeona yaliyokuwa yakiendelea kwenye mitandao ya kijamii siku za karibuni, sasa ile inaua sanaa, leo hata makampuni yaliyoanza kuwa na imani kibiashara na wasanii wameanza kusita tena, heshimuni sanaa ni maisha ya wengi na hii itawajengea heshima badala ya kutumia kiki za kuchafuana,” ameongeza Dkt. Abbasi.