Na Mwandishi Wetu,Timajimaraonline, Dar
SEPTEMBA 4-6, 2024 Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAS) uliofanyika jijini Baijing.
Katika Mkutano huo China ilitanga kuzipatia nchi za Afrika Dola za Marekani Bilioni 50 zitakazotumika kuwezesha utekelezaji wa maeneo 10 ya ushirikiano ambapo Dola bilioni 29 ni kwa ajili ya mikopo, Dola bilioni 11 ni kwa ajili ya misaada na Dola Bilioni 10 zitatolewa kwa njia ya kuwezesha uwekezaji kutoka China.
Akiwa nchini China Rais Dkt. Samia alikuwa na mazungumzo ya uwili kati yake na Rais wa China, Xi Jinping yaliyofanyioka Septemba 4, 2024, ambapo Rais Xi aliridhia kushirikiana na Tanzania katika miradi ya kusambaza umeme wa Kv 400, upanuzi wa hospitali ya JKCI, mradi wa kuzalisha malisho ya mifugo kwa teknolojia ya Juncao; kufufua reli ya TAZARA na mradi wa mtandao wa mawasiliano vijijini.
Miradi mingine ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, nishati safi ya kupikia, kuendeleza kilimo, uchumi wa buluu na kutekeleza miradi inayolenga kuunganisha nchi za Afrika na bahari ya Hindi kupitia Tanzania ili kuziunganisha na China.
Mkutano huo umeandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji; na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu na kuhudhuriwa na Makatibu Wakuu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Afisi ya Rais- Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar; Wizara ya Fedha, Viwanda na Biashara, Ujenzi, Uchukuzi, Utamaduni Sanaa na Michezo.
Wizara nyingine ni Mambo ya Ndani ya Nchi, Kilimo, Nishati, Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa na Afya.
Tayari Tanzania imeainisha njia na mbinu itakazotumia kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo FOCAC).
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, amebainisha hayo katika kikao cha Makatibu Wakuu kutoka Wizara 12 waliokutana kujadili namna ambavyo Tanzania itatekeleza makubaliano hayo ili kunufaika nayo.
Akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu yatokanayo na Mkutano huo Balozi Shelukindo amesema Tanzania itawasilisha miradi michache ya kipaumbele ambayo imefanyiwa tathmini na upembuzi yakinifu kwa mujibu wa muongozo wa Wizara ya Fedha na kuongeza kuwa kuwasilisha miradi hiyo kutasaidia kupunguza muda wa kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo.
Ameongeza kuwa Serikali itaainisha miradi mahususi ya uwekezaji na kufanya uhamasishaji kwa kampuni za China hususan za Kiserikali ili kuikubali miradi hiyo na hatimaye kunufaika na fedha za uwekezaji kiasi cha Dola Bilioni 10 zilizotengwa na Serikali ya China kwa ajili ya nchi za Afrika.
Anasema Serikali pia itaainisha bidhaa ambazo zinazalishwa nchini kwa wingi na kwa viwango vinavyotakiwa ambazo zitaingizwa kwenye soko la China na kuwezesha uzalishaji wa bidhaa hizo na usajili wa makampuni yatakayofanya mauzo ya bidhaa hizo nchini China.
“Serikali itafanya majadiliano na China ili kuingia makubaliano ya kufungua masoko kwa bidhaa zaidi kutoka Tanzania na kunufaika na hatua ya China kuruhusu bidhaa zote kutoka Afrika kuingia nchini humo bila kutozwa ushuru wa forodha” alisisitiza Balozi Shelukindo.
Amesema Serikali na Sekta binafsi zitachangamkia fursa za mafunzo na kubadilishana uzoefu zinazotolewa na China kwa wakati ili kuwawezesha Watanzania wengi kunufaika na fursa hizo.
Serikali pia itaishirikisha China katika masuala muhimu yanayojadiliwa kwenye taasisi za kimataifa ili kupata uungwaji mkono na China katika taasisi hizo na kusaidia kusukuma juhudi za upatikanaji wa fedha zinazotolewa kupitia taasisi hizo.
Anasema Tanzania ina fursa ya kipekee ya kunufaika na ahadi za FOCAC kutokana na uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na China ambapo China inaichukulia Tanzania kuwa ni nchi ya mfano katika uhusiano na ushriikiano wake na nchi za Afrika.
Awali akifungua mkutano huo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida alisema mkutano wa FOCAC 2024 umefungua fursa kwa bara la Afrika na kuongeza kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kuhakikisha inanufaika na fursa hizo zilizo katika maeneo matano makubwa ya viwanda, kilimo, miundombinu, biashara na uwekezaji.
Aidha alisema FOCAC 2024 imebainisha maeneo kumi za kiushirikiano baina ya China na nchi za Afrika ambayo ni Ushirikiano katika mafunzo; Kuimarisha ushirikiano katika ustawi wa biashara.
Maeneo mengine ni ya Kuimarisha ushirikiano katika viwanda; Ushirikiano katika miundombingu unganishi (connectivity); Ushirikiano katika programu za maendeleo; Ushirikiano katika afya; Ushirikiano katika kuendeleza kilimo; Kuanzisha ushirikiano katika utamaduni; Ushirikiano katika nishati ya kijani (green energy); na Ushirikiano katika ulinzi na usalama.
Akizungumza katika kikao hicho Balozi wa Tanzania nchini China, Dkt. Khamis Omar alisema FOCAC 2024 ni nafasi adimu ambayo imeiwezesha Tanzania kukuza uhusiano wake wa kidiplomasia na China na hivyo kukuza kasi ya maendeleo ya Taifa na kuongeza kuwa ni muhimu kwa maeneo yanaopendekezwa kupitia jukwaa hilo kuwasilishwa kwa haraka ili kuwezesha utekelezaji wake.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika