November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Elimu (Tamisemi ), Julius Nestory akizungumza na waratibu elimu kata,walimu wa darasa la awali na walimu wakuu (hawapo pichani) wa Halamshauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma,kulia kwake ni Mkurugenzi wa CiC, Creig Ferla na kushoto kwake ni mwezeshaji wa mafunzo kutoka CiC Frank Samson. (Picha na Joyce Kasiki).

Waratibu elimu,walimu wakuu watakaotimuliwa kazini watajwa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira Online,Dodoma

MKURUGENZI wa Elimu ,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Julius Nestory amewataka walimu wakuu,waratibu elimu kata na maafisa elimu kata katika Wilaya ya Kongwa na Chamwino kuhakikisha wanatenga madarasa mazuri na yenye vifaa kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wa darasa la awali.

Akizungumza na viongozi hao pamoja na walimu wa madarasa ya awali waliokuwa wakipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kutoa elimu bora kwa wanafunzi wa darasa la awali,Mkurugenzi huyo amesema,kwa viongozi watakaoshindwa kufanya hivyo wataondolewa kwenye nafasi walizo nazo.

Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo viongozi wa elimu kata na walimu wakuu wa shule za msingi yamefadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la kusaidia watoto wanaopitia changamoto mbalimbali (CiC) ambalo linatekeleza mradi wa Watotowetu Tunu yetu katika wilaya ya Kongwa na Chamwino mkoani Dodoma.

“Tayari tulishatoa maelekezo kwamba viongozi wa kata husika kwa kushirikiana na mwalimu mkuu wa shule,wanapaswa kutenga darasa zuri lenye mlango na madirisha yanayofungwa na lililowekwa zana na kufundishia na ujifunzaji wa watoto wa darasa la awali.

“Sasa leo mmepewa mafunzo na mmeonyeshwa darasa la mfano la wanafunzi wa awali linavyotakiwa kuwa,lina kona zote za ujifunzaji,lina vifaa na michezo mbalimbali inayomwezesha mtoto kujifunza,sasa nitashangaa kupita kwenye maeneo yenu yasiwepo hayo,niwaambie tu mtaondoka,”amesema.

Kwa upande wake Kamishina wa Elimu,Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Dkt.Lyabwene Mtahabwa amesema,wahusika wa mradi katika wilaya hizo wautendee haki mradi huo na wanafunzi na walimu kutoka shule ambazo hazijapata mradi wakajifunza kwao.

Kamishina wa Elimu,Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Dkt.Lyabwene Mtahabwa. (Picha na Joyce Kaisiki)

“Mapinduzi ya maendeleo endelevu katika elimu ya awali yaanze Dodoma katika wilaya ya Kongwa na Chamwino,tunataka kuona walimu,wanafunzi na viongozi wengine wanakuja kujifunza kwenu,”amesema Dkt.Mtahabwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa CiC, Creig Ferla amesema, mafunzo hayo yamelenga kupata mabalozi kwa elimu ya awali ,makuzi na maendeleo ya mtoto lakini pia kuwajengea uwezo walimu na kuwapa ari ya ufundishaji madarasa ya elimu ya awali.

Amesema,shirika hilo limeamua kuwekeza katika elimu ya awali ili kuwapa watoto msingi mzuri wa elimu mara tu wanapoanza shule.