November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wapewa Mbinu za Kuepuka Kuzama Majini

Na Fresha Kinasa, Timesmajira Online, Musoma 

Zaidi ya wavuvi 9,000 wanaoishi katika mialo ya Kome na Busekera, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, wameelimishwa kuhusu usalama majini. 

Elimu hii inatolewa na Shirika la Environment and Economic Development Organization (EMEDO) katika mradi wa ‘Kuzuia Kuzama Ziwa Victoria’, kwa ufadhili wa Taasisi ya Royal National Lifeboat Institute ya Uingereza.

Mradi ulianza mwaka 2021 baada ya utafiti ulioonesha hatari zinazohusiana na kuzama majini, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa elimu ya usalama, vifaa vya kujiokolea, na tabia za wavuvi kuingia majini wakiwa walevi.

Hayo yamebainishwa  na  Septemba 23,2024, na Ofisa Mradi wa huo kutoka EMEDO,Majura Maingu,wakati akizungumza  na Timesmajira Online,katika maadhimisho ya siku ya Usafiri wa Maji Duniani na miaka 50 ya uanachama wa Shirika la Bahari duniani (IMO) yanayofanyika kitaifa,uwanja wa shule ya msingi Mukendo Manispaa ya Musoma.

Maingu,amesisisitiza umuhimu wa elimu hiyo, huku akielezea kuwa wavuvi sasa wanatumia makoti okozi na wameshirikiana na viongozi wa maeneo husika kuunda sheria za usalama.

Pia, EMEDO imeanzisha maadhimisho ya kuzuia kuzama majini ifikapo Julai 26 ya  kila mwaka, ikishirikiana na mamlaka mbalimbali za usalama.Ikiwemo Maofisa Uvuvi, TASAC, TMA, Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, BMU pamoja na Wizara mtambuka zinazohisiana na usalama majini.

Wananchi sasa wanatumia makoti ya bei nafuu, yaliyotengenezwa kwa chupa za maj ambayo ya auzwa kwa shilingi 8,000, na hatua hizi zimeongeza uelewa na usalama wa wavuvi.Huku makoti  mengine ya kawaida yanauzwa kati ya shilingi 30,000, 50, 000 hadi 60,000.

Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya, amepongeza ubunifu huo wa kutumia chupa za maji kutengeneza  makoti ya uokozi kwa gharama nafuu huku akiitaka jamii kuzingatia sheria za usafiri majini.

Mwenyekiti wa BMU Mwalo wa Kome Kata ya Bwasi,Piud Masige amesema kuwa, Mradi wa ‘Kuzuia kuzama Ziwa Victoria’ umeleta manufaa kwa Wavuvi na Wananchi ambapo awali kabla ya Mradi huo. Uelewa kwa Wananchi ulikuwa mdogo na pia hawakuzingatia uvaaji wa Makoti okozi wanapofanya shughuli za uvuvi. 

Akizungumza katika banda la EMEDO  katika maadhimisho hayo,Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukizi Zanzibar,Makame M. Haji amepongeza kazi ya utoaji wa elimu kwa wananchi iliofanywa na shirika hilo. Huku akiomba liendelee kuwafikia wengi zaidi hasa ikizingatiwa Mkoa wa Mara una idadi kubwa ya Wananchi wanaotumia usafiri wa majini.