November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wapatiwa vifaa ili kutokomeza udumavu

Na Edna Alex,TimesMajira Online. Singida

KATIKA harakati za kuhamasisha jamii juu ya lishe bora na kutokomeza hali ya udumavu Mkoa wa Singida, Shirika la SEMA mkoani hapa kwa kushirikiana na Shirika la Rekoda kupitia Mradi wa ‘Boresha Lishe’, wametoa vifaa kwa wahamasishaji wa lishe vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 49.

Vifaa vilivyotolewa ni baiskeli 97 na vipaza sauti 97 vyenye thamani ya sh. 49,945,000 kwa wahamasishaji lishe kutoka katika vijiji 85 vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya ya Singida na Ikungi mkoani hapa.

Akifungua kikao hicho cha makabidhiano ya vifaa hivyo kilichofanyika katika Ukumbi wa RC Mission mjini hapa Meneja wa SEMA, Ivo Manyaku ameushukuru uongozi wa Serikali ya Mkoa kwa ushirikiano walioupata tangu walipoanza mradi huo mwaka 2007.

“Huu mradi unalenga kuwapa elimu ya lishe bora wananchi wa mkoa wetu, ili waondokane na udumavu hali itakayosababisha kuongezeka uzalishaji mali na hatimaye kuinua vipato vya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema.

Akipokea vifaa hivyo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi ameyapongeza mashirika hayo kwa mradi huo na kuwataka wahamasishaji hao waliolengwa kupewa vifaa hivyo, kwenda kuvitumia vizuri na kuvitunza ili visaidie kupunguza udumavu kwa jamii husika.