Na Sophia Fundi, Timesmajira Online,Karatu
Wananchi wilayani Karatu mkoani Arusha wameiomba Halmashauri ya Wilaya hiyo kuboresha miundombinu ya barabara hasa mifereji ya kutolea maji ya mvua ili kukabiliana na athari zinazotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kauli hiyo ya wananchi imekuja baada ya mvua kubwa kunyesha zaidi ya masaa manne na kusababisha uharibifu wa bidhaa kwa baadhi ya wafanyabiashara katika maeneo ya Gilala na Stend Kuu ya Karatu.
Akizungumza na wanahabari mmoja wa wafanyabiashara wa maeneo hayo Paulo Kivuyo amesema kuwa mifereji iliyoko ni midogo na kushindwa kuhimili maji yanayotoka maeneo mbalimbali hivyo kusababisha uharibifu wa mali.
“Mifereji na kalavati mnayoiona ni midogo sana imesababisha maji kushindwa kupita na kusambaa ambapo yameingia kwenye maduka na nyumba za watu mnavyotuona tunatoa vitu nje vimeloana na magodoro mnaona tumeanika juu ya bati sijui ikirudia kunyesha baadaye tunafanyeje,tunaomba serikali itusaidie kupanua kalavati,”amesema Kivuyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Juma Hokororo amewapa pole wananchi wote ambao mali zao zimeharibiwa na mvua huku akiwataka kutotupa taka ovyo kwenye mitaro ya kupitisha maji ya mvua kwani ndio chanzo kikuu cha athari hizo pamoja na kuwasisitiza kuendelea kuchukua tahadhari.
Amesema kuna tabia ya watu wanatupa mifuko mikubwa ya taka wakati mvua inanyesha ambapo inasababisha mitaro kuziba hivyo amewaonya watu kuacha tabia ya kutupa taka ovyo hasa wakati wa mvua.
Amewataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ya uwepo wa mvua za El-nino.
Aliwahimiza watu walioko mabondeni kuchukua tahadhari ya kuhama pamoja na kuacha kutembea nyakati za mvua.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi