January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waomba fomu zenye maandishi ya nukta nundu

Na Ashura Jumapili,TimesMajira online Kagera

Watu wenye ulemavu wameomba mamlaka husika inayosimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa,kutoa fomu za kugombea na kupigia kura,zenye maandishi rafiki kwao.

Ambapo fomu hizo ni pamoja na zenye maandishi ya nukta nundu kwa ajili ya watu wenye uoni hafifu, ili waweze kupata haki yao ya kikatiba ya kugombea na kuchagua viongozi.

Hayo yamesema Septemba 26,2024, na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Uemavu, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ,Novart Mwijage, baada ya kikao cha Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri hiyo, cha kutoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa wadau mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu,viongozi wa dini,wanasiasa,wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na wasanii,kilichofanyika mkoani Kagera.

Mwijage,amesema fomu za kugombea na kupigia kura zinatakiwa kuwa na mfumo rafiki, ili wakati wa kupiga kura, watu wasioona waweze kupiga kura, bila kumtegemea mtu mwingine ikiwa ni sehemu ya haki yake ya kikatiba kumchagua kiongozi anayemtaka.

Pia ametoa wito,kwa watu wenye ulemavu, wakijitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa,huku akihimiza kuwa wapewe kipaumbele,huku akieleza kuwa bado jamii haijaelewa kuwa mtu mwenye ulemavu anaweza kuingiza vizuri.

‘’Uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa mwaka 2019,niligombea nafasi ya ujumbe,kwa sababu nilikuwa na sifa na uwezo wa kuongoza wananchi wenzangu ‘’anasema Mwijage.

Sanjari na hayo, ameeleza kuwa,watu wenye ulemavu wapo tayari kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa,kwa kugombea na kupiga kura, hivyo anakwenda kuwahamasisha wenzake ili wajitokeze kwa wingi.

Awali Msimamizi wa Uchaguzi,Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba,Jacob Nkwera,ametoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mujibu wa kifungu cha 87 ‘A’ya sheria ya serikali za mitaa.

Nkwera,amesema maelekezo hayo yanatakiwa kutolea siku 62,kabla ya kufanyika kwa uchaguzi,lengo ni kuhakikisha,taratibu zote zinafuatwa kwa wagombea pamoja na wapiga kura,wanapata taarifa zinazohitajika kwa wakati.

Amesema, maelekezo hayo yanatoa taarifa ya mchakato wa uchaguzi, kuanzia uandikishaji na kupiga kura.Ili kuhakikisha uchaguzi, unafanyika kwa uwazi ,haki na usawa kwa kuzingatia sheria ya uchaguzi.

Pia amesema,zoezi la kujiandikisha katika daftari la makazi,litaanza Oktoba 11 hadi 20,mwaka huu kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa 12 kamili.

“Vyama vya siasa, vinaruhusiwa kuweka mawakala kwenye vituo,wakati wa zoezi la uandikishaji,katika daftari la makazi la mtaa kwa gharama zao,”amesema.

Amesema,kwa mujibu wa kanuni 31, uchaguzi utafanyika katika mtaa husika,huku mtu mwenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea,rai wa Tanzania,mkazi wa mtaa husika,mwenye akili timamu na amejiandikisha kupiga kura anastahili kushiriki kupiga kura kuchagua kiongozi anayemtaka.

Hata hivyo,amesema, mtu yoyote mwenye miaka 21, anaruhusiwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo,lakini awe mkazi wa mtaa husika na raia Tanzania,mwanachama wa chama cha siasa,na adhaminiwe na chama chake.

Amesema,fomu za ugombea, zitatolewa na kurudishwa kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi,Novemba 1 hadi 7,mwaka huu,itakuwa na nembo ya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, zitatolewa mtaa husika bila masharti yoyote wala malipo.

Uteuzi wa wagombea utafanyika Novemba 8,2024, baada ya zoezi hilo Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi, atabandika majina ya watu wenye sifa na wasiokuwa na sifa kwenye mbao za matangazo.

Aidha amesema pingamizi dhidi ya wagombea zitatolewa,Novemba 8 hadi 9,2024,huku maamuzi ya pingamizi yatatolewa Novemba 9 hadi 10,),huku zoezi la kampeni litaanza Novemba 20 hadi 26,mwaka huu.Uchaguzi unatarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.

Kwa upande wake,Mbuge wa Bukoba Mjini,Wakili Steven Byabato,amewahimiza anasema vijana na wanawake,kujitokeza kwa wingi, kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kugombea na kupiga kura.