Na Reuben Kagaruki, TimesMajiraOnline, Chato
“TUNAMUOMBA Rais Samia Suluhu Hassan, aendelee kuisimamia TASAF (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii) ili iweze kusaidia Watanzania wengi.
Wanakijiji wanaona maisha yangu yamebadilika, hata nafasi ya kuuliza swali kwenye mkutano wa Kijiji siku hizi napewa. Namuomba Mama Samia azidi kuusimamia mfuko huu uendelee kuwa imara unatusaidia sisi maskini.”
Hiyo ni kauli ya Ashura Deus Rushona (36) Mkazi wa Kijiji cha Nyakato, Kata ya Bukome, Wilaya ya Chato mkoani Geita, aliyoitoa wakati akitoa ushuhuda jinsi Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulivyobadilisha maisha yake kupitia ruzuku anayopewa.
Anaongeza kuwa; “Nashukuru TASAF imenifanya niwe na thamani mbele ya jamii, zamani nilipokuwa naenda kwenye mkutano wa kijiji hata niliponyosha mkono sikupewa nafasi ya kuzungumza.
Hata nilipopewa nafasi, hoja yangu haikujadiliwa, watu walikuwa wanaona huyu maskini atasema nini, lakini baada ya TASAF kubadilisha maisha yangu, naonekana wa thamani.
Kauli ya Ashura inabeba hisia za wanawake wengi ambao wamenufaika na TASAF kwa kuwaondoa kwenye hali ya umaskini waliokuwa nao na sasa hivi wanaishi maisha ya raha, ambayo hawakuyategemea kabisa.
Anasema zamani hakuwa hivyo, alivyo sasa, amekuwa hivyo kwa sababu ya TASAF, hivyo anamuomba Rais Samia aendelee kuhakikisha mfuko huo unasaidia watu wengi zaidi wenye uhitaji.
Anasema kabla ya kuanza kupata ruzuku ya TASAF, iliyomuwezesha kuanzisha shughuli za kumuingizia kipata alikuwa anaishi maisha magumu, ilikuwa vigumu kwake kuhudumia watoto wake watatu.
Kati ya watoto hao, wawili walikuwa wanasoma na wakati mwingine walikuwa wanaenda shule bila kuvaa hata kandambili na hawakuwa na sare za shule.
“Hata chakula ilikuwa ni shida, nilikuwa nanunua koronto moja la mahindi (kopo la kilo moja la mahindi ya kusaga) nasaga mchana na usiku tunakula, tulikuwa hatushibi na wakati mwingine tulilala njaa, chakula sikuwa nacho ndani,” anasema Ashura.
Wakati huo pia anasema alikuwa anaishi kwenye chumba kimoja kwenye nyumba ya udongo iliyoezekwa kwa nyasi.
Anasema alianza kunufaika na mpango huo mwaka 2015, ambapo alianza kupokea ruzuku iliyomuwezesha kununua nguo za watoto za shule.
Aidha, anasema kwenye fedha alizopewa alibakiza kiasi kidogo alichokitumia kununua nyanya kwa wakulima na kwenda kuuza kwa bei ya rejareja sakoni.
Baada ya kuuza nyanya, faida aliyopata alinunua kuku na bata na kuanza ufugaji.
Kwa mujibu wa Ashura, taratibu maisha yake yalianza kubadilika leo hii ana uhakika wa chakula ndani, anafanya biashara ya kuuza nyanya, ambapo kwa siku ananunua madumu matano na kwenda kuuza sokoni kwa bei ya rejareja.
Anafafanua kuwa fedha anazopata kwenye nyanya ameanzisha mradi wa ufugaji kuku na bata wakizaliana anauza ananunua chakula. Bi. Ashura anasema kwa sasa ana kuku 62 na bata 19.
Anaongeza kuwa faida nyingine anayopata kwenye miradi hiyo, inamsaidia kusomesha watoto na halali njaa tena.”Nilikuwa nalala chini, lakini leo nalala pazuri,” anasema na kuongeza; “Maisha yangu yanakwenda vizuri kupitia mpango wa TASAF.
Anasema kwa sasa amehama kwenye nyumba ya nyasi, amepanga vyumba viwili na sebule na nyumba imesakafiwa na ina umeme na imeezekwa kwa bati.
Lakini pia, anasema amejiunga kwenye kikundi cha kuweka akiba cha Mkombozi, ambacho kina wanachama 14, ambapo wamekuwa wakinunua hisa sh.1000 na kuweka akiba ya sh. 2,000 kila wiki, ambapo kwa sasa wana akiba ya sh. 3,074,000.
Kwenye kikundi hicho, anasema yeye alishakopa sh. 370,000 na kuongeza kwenye mtaji wake nyanya. Kwa mujibu wa Bi. Ashura mtaji wake wa nyanya ni sh. 300,000 huku ule kuku na bata akiwa alianza na sh. 100,000.
Pia, anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata Ruzuku ya Uzalishaji ambapo yeye amepewa mbuzi watatu. Anasema mmoja amezaa na anaamini mbuzi hao watamsaidia kumuongezea kipato ili baadaye aweze kununua mabati aanze ujenzi.
Mnufaika mwingine, Kulwa Mavano (40) Mkazi wa Kijiji Zumangabo, Kata ya Bwanga Wilaya ya Chato, mkoani Geita, anasema kutokana na usimamizi imara wa Rais Samia kwenye mfuko wa TASAF, ameweza kuwa na kipato cha uhakika hadi mumewe aliyemkimbia kwa sababu ya umaskini kumrudia na kuanza kumpigia magoti ili warudiane.
Hata hivyo anasema amekataa kurudiana na mume wake, akisema; “Anataka turudiane kwa sababu anaona Rais Samia amenitoa kwenye maskini! Naendelea kupambana mwenyewe, kwa sababu Serikali ya Mama Samia kupitia TASAF imeniwezesha,” anasema Kulwa.
Kwa mujibu wa Kulwa, mumewe amefikia uamuzi huo baada ya kuona hali yake ya maisha imebadilika na sio maskini tena.
“Ameona nimejenga nyumba, nasomesha watoto, napendeza kwa sababu ya TASAF, ndipo anataka turudiane, nimemkatalia,” anasema Kulwa.
Anasema kabla ya kujiunga na TASAF alikuwa na hali ngumu (alikuwa anaishi kwa kufanyakazi vidaladala (kazi za kulipwa kwa masaa).
Kwa mujibu wa Kulwa hali ilikuwa mbaya zaidi pale alipotelekezwa na mume wake na ilifika hatua watoto walikuwa hawaendi shule.
“Sikuwa na uhakika hata wa kula, hivyo hata watoto walikuwa hawaendi shule,”anasema.
Anasema anamshukuru Rais Samia kwa kuwatoa katika maisha magumu, kwani kupitia TASAF amewezesha familia yake kutoka kwenye hali ngumu ya maisha.
Anasema biashara ya kuuza mkaa imemwezesha kujenga nyumba na kuwa na uhakika wa kusomesha watoto, kuwapatia matibabu na mahitaji mengine muhimu.
Kulwa anasema amepata mafanikio hayo baada ya kuingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Anasema baada ya kuingia TASAF na kupata ruzuku ya kwanza ya sh. 40,000 alichukua sh. 30,000 akaanzisha biashara ya kuuza mkaa.
Anasema alianza na mtaji wa gunia mbili, lakini kadri alivyokuwa akipata fedha za TASAF alizidi kuongeza mtaji, ambapo hadi sasa ana mtaji wa gunia tano na kwa upande wa fedha, mtaji wake ni sh. 200,000.
“Mkaa wangu nauza kwa kupanga mafungu, fungu moja sh. 500 na kama biashara imekubali kwa siku ninauza mkaa wa sh. 20,000 hadi 30,000,” anasema Bi. Kulwa.
Kwa mujibu wa Kulwa baada ya kuanzisha biashara hiyo, maisha yake yalianza kubadilika, akawa na uwezo wa kusomesha watoto wake vizuri, kuwanunulia nguo na maisha nyumbani yakawa mazuri.
Anaeleza kwamba tayari watoto wake wawili wamemaliza darasa la saba na wengine wanaendelea na masomo.
Aidha, anasema ana uhakika wa kuwapatia watoto wake matibabu na uwezo huo umetokana na biashara yake ya kuuza mkaa.
Mbali na kusomesha watoto, Bi. Kulwa anasema faida aliyokuwa anapata ilimwezesha kununua kiwanja na mabati kujenga nyumba.
“Kabla ya TASAF sikuwa na nyumba, lakini leo hii nipo kwangu,” anasema. Kinachomfurahisha sasa ni jinsi TASAF ilivyomfanya aaminike ndani ya jamii.
“Kabla sijapata ruzuku ya TASAF hata nilipoenda kumkopa mtu hela, nilikataliwa, lakini sasa hivi kila ninayemkimbilia ananikopesha maana anajua nina biashara, nitalipa,”anasema Bi. Kulwa na kuongeza;
“Kipindi cha nyuma nilikuwa hata sipewe kadi ya mchango wa harusi, lakini leo hii naalikwa kwa sababu wanajua nina uwezo wa kuchangia.”
“Ningesimama wapi wakati nilikuwa nimekondeana, nanuka shida, wangenipa kadi wakati sina cha kuchangia, lakini sasa ndani ya jamii nasikilizwa,” anasema, Kulwa.
Mbali na kuwa na biashara ya mkaa, Kulwa anasema ameanzisha mradi mwingine wa ufugaji mbuzi kupitia faida aliyokuwa akiipata kwenye mkaa, ambapo kwa sasa ana mbuzi saba.
“Nilikuwa nimeishafikisha mbuzi 10, watatu wamekufa, wamebaki saba, hao ndio akiba yangu nikiwa na shida nauza mmoja natatua shida yangu,” anasema.
Mbali na mbuzi, anasema anajishughulisha na kilimo, njugu mawe, mihogo na hivyo kwa mwaka mzima anakuwa na uhakika wa chakula.
Naye Spensioza Sono (47) mkazi wa Kijiji cha Msilale Kata ya Chato, Wilaya ya Chato, mkoani Geita, anamuomba Rais Samia kuendelea kuuwezesha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili uzidi kuwainua Watanzania wenye hali duni ya maisha ili waweze kuwa na uchumi imara kama ilivyofanyika kwake.
Spensioza alitoa kauli hiyo wakati akieleza jinsi mfuko huo ulivyomuinua kiuchumi na kubadili maisha yake.
Spensioza ambaye nyuma yake wapo Watanzania wengi, ambao hali zao za kiuchumi zimeimarika kupitia ruzuku ya TASAF, anasema aliingizwa kwenye mpango huo miaka saba iliyopita, wakati huo akiwa na hali duni kiuchumi.
Mama huyo mwenye watoto nane, anasema wakati anaingizwa kwenye mpango huo alikuwa akiishi kwenye nyumba ya tope ya vyumba viwili, alikuwa na mtaji wa sh. 20,000 ambao haukumuwezesha kupata kipato cha kutunza familia, kusomesha watoto, kuwapatia matibabu na hata kijijini kwao alijulikana kama mtu duni, ndiyo maana mkutano wa kijiji uliamua aingizwe kuwenye mpango wa TASAF.
“Mimi ni mwanamke jeshi moja, sina mume, lakini naishukuru Serikali kwa kutuletea Mpango wa TASAF, kwa kweli umenitoa, nilikuwa na maisha duni.
Akithibitisha kwa nini anamuomba Rais Samia, aendelee kuhakikisha TASAF inakuwepo ili isaidie watu wengi zaidi, anasema baada ya kuingizwa kwenye mpango huo na kupewa ruzuku alianza aliitunza na alipofikisha kiasi alichokusudia alinunua mbuzi.
Anasema mbuzi walipozaliana, aliuza na fedha alizopata aliziingiza kwenye mtaji wa biashara yake ya kuuza nafaka.
Kupitia mtaji huo anasema alianza kuuza nafaka za aina zote zikiwemo za karanga, maharagwe, ufuta, mahindi, mtama, njungu, njegele na soya.
Anasema kadri alivyokuwa akipata ruzuku ya TASAF, alizidi kuongeza mtaji pamoja na faida aliyokuwa akipata hadi mtaji wake umefikia sh. milioni 4.5 kutoka sh. 20,000.
Mafanikio hayo, ndiyo yalimfanya ahame kwenye nyumba ya tope ya vyumba viwili na kujenga nyumba ya vyumba vinne ya tofali za kuchoma.
Kwa mujibu wa Spensioza nyumba hiyo imeezekwa kwa bati, ndani chini imesakafiwa, amevuta umeme na maji na ana televesheni.
Aidha, anasema amejenga nyumba nyingine mpya ya tofali za block yenye vyumba nane, ambayo nayo ni matokeo ya TASAF.
“Ukifika nyumbani kwangu mimi ni mama kweli kweli, nalala vizuri na watoto wangu,” anasema Spensioza. “Siku hizi watoto wanalala kwenye vitanda, wanalalia magodoro mazuri na wanapata elimu bila wasiwasi, nawanunulia nguo, viatu na daftari.”
Anasema mtoto wake mmoja amemsomesha kwa nguvu za TASAF na amefaulu na kuchaguliwa kuendelea na masomo mkoani Mbeya, shule ya vipaji maalum.
Aidha, anasema ana watoto wengine ambao anaendelea kuwasome, ambapo mmoja anamlipia ada ya sh. milioni 1.5 na yule anayesoma Mbeya licha ya nauli ya kutoka Chato kwenda shuleni anakosoma kuwa kubwa, lakini hana wasiwasi wa kuipata.
Aidha, anasema TASAF imemfanya awe mtu wa thamani ndani ya jamii, akisema; “Kabla sijaingizwa kwenye mpango huu nilikuwa sina mwonekano mzuri, nilikuwa na maisha magumu, kwenye jamii nilikuwa naonekana mtu wa namna gani!”
Lakini baada ya kuwezeshwa na TASAF nikawa na mwonekano mzuri kama mwanamke anayekaa kwenye mazingira mazuri niligombea uongozi na wananchi walinichagua.
Hapa nilipo ni mama niliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Tawi la Msilale CCM, vile vile alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa kupitia ngazi ya Kijiji cha Msilale.
Aidha, anasema amejiunga na vikundi ambavyo vimesajiliwa na halmashauri, ambapo kwenye kikundi chao wana ufugaji wa mbuzi na wakishazaliana wanauza wanagawana fedha kwa ajili ya maendeleo ya familia.
Katika kikundi hicho, kila mwezi anasema wanakutana mara moja na kila mmoja anaweka akiba ya sh. 10,000 ambazo zinakusanywa na kupewa wale wanaotaka mkopo.
Anasema ndani ya kikundi hicho, mikopo wanayokopeshana inaanzia sh. 300,000 hadi sh. milioni 1, ambapo yeye Julai mwaka huu alikopa sh. 700,000 ambazo amezitumia kununua shamba kwa ajili ya kilimo, hivyo hatarajii tena kukodi mashamba kwa watu.
Aidha, anasema ana kikundi kingine cha wanawake wanufaika wa TASAF ambacho wanakutana mara moja kila wiki, ambapo wananunua hisa moja kwa sh. 500 na wanakopeshana asilimia 10.
Anasema Juni, mwaka huu walivunja wakagawana kila mmoja sh. 400,000 ambazo zimemsaidia kulipa ada ya watoto.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani