January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanufaika Mpango wa TASAF Igagara
wapiga hatua, sasa tayari kuhitimu

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline, Wanging’ombe

BAADHI ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Igagara Halmashauri ya Wilaya Wanging’ombe mkoani Njombe, wamesema wako tayari kuhitimu na kuondoka kwenye mpango huo unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kutokana na hali zao kiuchumi kuimarika.

Wanufaika hao ambao wamekuwa kwenye mpango huo kwa miaka nane, walitoa ushuhuda huo Februali 15, mwaka huu walipokuwa kwenye ofisi za kijiji cha Igagara kwa ajili ya kupokea ruzuku inayotolewa mfuko huo.

Wanufaika hao walipoulizwa na Afisa Maendeleo ya Jamii na Mhamasishaji Ngazi ya Wilaya wa TASAF,Ayoub Msigala, ni wangapi wako tayari kuhitimu wajitokeza hadharani na kutoa ushuhuda wa hali waliyonayo kwa sasa ikilinganishwa na kabla ya kuingizwa kwenye mpango huo.

Mkazi wa Kijiji cha Igagara, Veronica Mtewele (27) alisema kwa sasa yuko tayari kuhitimu na kuondoka kwenye mpango huo kwa sababu hali yake ya kiuchumi imeimarika.

Amesema kupitia mpango huo wa TASAF amejenga nyumba ya vyumba vinne ambayo ameezeka kwa bati na amepanda parachichi miche isiyopungua 20. Amesema wakati TASAF inaanza ilimkuta anaishi kwenye nyumba ya nyasi na maisha yake yalikuwa duni baada ya kifo cha baba yake.

Wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Igagara Halmashauri ya wilaya Wanging’ombe mkoani Njombe wakisubiri malipo ya ruzuku kutoka TASAF

Anasema mbali na kuwa na miche ya parachichi, analima viazi, mahindi, njegere na ngano. “Kwa hiyo nawashauri wenzangu tunapopata hizi fedha kutoka TASAF tunaweza kuziona ni ndogo, lakini ukizifanyia bajeti unaweza kufanya vizuri na kufikia hatua ya kuomba mwenyewe kuhitimu kwenye mpango,” anasema Mtewele.

Anaongeza kwamba yeye anaposema TASAF imemsaidia kitu fulani, kinaonekana kwa macho kwamba alifanyi hivi na hivi na hiki ndicho kilipatikana.

Alitoa mfano kwamba baada ya kupata ruzuku kutoka TASAF yeye na wenzake walianzisha kikundi wakawa wanakopeshana , hivyo ilipofika zamu yake wa kukopa, mkopo aliokuwa akipata alinunua vifaa vya ujenzi hadi akafanikiwa kujenga nyumba hiyo.

Naye Ephram Mgaya (54) anasema anaishukuru TASAF, kwa sababu imewasaidia dada zake wawili wenye ulemavu, ambapo wameanzisha miradi ya ufugaji nguruwe na wamepanda parachichi, hivyo wana uhakika wa kupata mavuno endelevu.

Wanufaika wa Mpango wa TASAF

Anasema awali ilikuwa ni vigumu kwake kuwahudumia, lakini TASAF imewasaidia sana, kwani sasa hivi hawamtegemei kama ilivyokuwa kabla ya kuingizwa kwenye mpango huo.

Naye Aida Mtotoma (60) anasema anaishukuru TASAF kwa sababu wakati anaingizwa kwenye mpango ho hali yake ilikuwa mbaya na alikuwa hana nyumba ya kuishi.

Anasema baada ya kuingia kwenye mpango alitumia fedha za ruzuku alizokuwa anapewa kuanzisha miradi ya ufugaji kuku, mbuzi na sehemu ya fedha alinunulia mbolea kwa ajili ya kilimo.

Anasema alianza kupata kipato kilichomwezesha kujenga nyumba ya vyumba vitatu aliyojenga kwa tofali za kuchoma na kuiezeka kwa bati. “Naishukuru sana TASAF kwa kunifikisha hapa kwa sababu imenitoa kwenye shida,” anasema.

Naye Matrida Nyigu (70) anasema TASAF imemwezesha kuanzisha miradi ya ufugaji, amejenga nyumba na fedha anazopata ananunua mbolea kwa ajili ya kuweka kwenye shamba lake la viazi na mahindi.

Mnufaika wa Mpango wa TASAF katika kijiji cha Igagara akiandaliwa malipo yake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Igagara,Isdory Sambula, anaishukuru TASAF kwa kazi kubwa ambayo imeanyika kwenye kijiji chake, kwani hali ya wanufaika wa mpango huo wapatao 80 imebadilika ikilinganishwa na kipindi ambacho walikuwa hawajaingizwa kwenye mpango huo.

“Kwa kweli mabadiliko yapo ni makubwa kama ambavyo umesikia mwenyewe wengine wanasema wako tayari kuhitimu,”anasema na kuongeza;

“Wengine wamepanda parachichi na wengine wanasema wapo tayari kuhitimu.”

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii na Mhamasishaji Ngazi ya Wilaya wa TASAF,Ayoub Msigala, alisema tangu 2015 walipoanza kupata ruzuku hadi sasa ni miaka 8 na hata mtoto wa darasa la kwanza aliyeanza shule ya msingi ameishahitimu.

“Wewe ni nani jamani usihitimu?” Alipotaka kujua ni wangapi wapo tayari kuhitimu waliokuwa tayari walinyosha mikono na kuita mmoja mmoja na kutoa ushuhuda wa kwa nini yuko tayari kuhitimu.

Msigala anasema mafanikio hayo ndiyo dhana ya TASAF ya Kunusuru kaya za walengwa.

“Kwa hiyo nia ya mpango huu ni kuona watu wanapiga hatua , pale walipokutwa isiwe leo, leo ni siku nyingine . Kama walikuwa hawali milo mitatu, basi wale milo mitatu, kama watoto walikuwa hawaendi kliniki, basi waende kliniki, kama walikuwa hawaendi shule, basi waende shule,” anasema Msigala.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TASAF, Zuhura Mdungi aliwapongeza walengwa wa mpango huo ambao wako tayari kuhitimu, kwani hilo sio suala baya, bali wanaonesha kwamba fedha walizokuwa wakizipata walizifanyika kazi na kutoka kwenye hali waliyokuwa nayo na kuwa kwenye hali nyingine kabisa.

“Kuna dada hapa amesema amejenga nyumba yake nzuri ana miti ya miparachichi, lakini najua wengine wengi mna vitu kama hivyo, hivyo mnastahili kujipongeza,” anasema Mdungi.

Anasema unapofikia kuhitimu ina maana tayari umepiga hatua ili siku nyingine linapokuja zoezi la kutambua walengwa, huyo mtu hatatajwa.

“Si mnakumbuka wakati wanawatambua vigenzo vilivyokuwa vinatumika? Kwa hiyo sasa wakija wakasema tuje tutambue wengine wote hapa mtakuwepo?”Alihoji Mdungi na kujibiwa kwamba hawatakuwepo kwa sababu ile hali ngumu waliyokuwa nayo watakuwa wameachana nayo.

Anasema huo utaratibu watakuwa wakienda nao hivyo hivyo, ingawa sio watu wote wataambiwa ondokeni kwa sababu wamekuwa kwenye mpango wa muda mrefu, kwani wanajua kuna wazee sana ambao kwa hali zao wanaonekana wanahitaji kuendelea kusaidiwa.

Wanufaika wa Mpango wa TASAF wakizungumza na mwandishi wa habari kuhusiana na mafanikio ambayo wamepata tangu walipojiunga na mpango huo.

“Hao wanaweza kuendelea kuwepo kwenye mpango ili kuendelea kuwasaidia, lakini wengine ambao hali zao zimekuwa nzuri hawatakuwa na sababu ya kuendelea kuwa kwenye huo mpango,” anasema.

Anasema hata kwenye kuhitimu darasa la saba kuna wengine wanafaulu, wengine wanashindwa na hata wengine kurudia mtihani? “Basi pia na huku kwenye mpango huu ni hivyo hivyo , wengine wataondoka, wengine wataondoka mwaka unaofuatia na wengine watakuwepo kidogo na wengine watajitoa wenyewe watasema jamani sisi hapa tulipofikia inatosha, tunaondoka kama wengine walivyosema hapa,” anasema Mdungi.

Anawataka kuendeleza miradi yao ambayo wanaifanya kwenye kilimo, ufugaji, biashara kwa sababu shughuli hizo ndiyo mkombozi wao.

Anafafanua kwamba Serikali itafurahi sana kusikia Igagara walengwa 80 waliokuwepo, walengwa 65 wote wamehitimu.

mWISH