March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanufaika mikopo ya asilimia 10 Temeke waswma imewakomboa kiuchumi

Na Irene Clemence,Timesmajira

BAADHI ya wajasiriamali walionufaika na mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmshauri ya Manispaa ya Temeke wamesema imewakomboa kiuchumi na kukuza biashara zao .

Wakizungumza katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea wajasiriamali kutoka
Kikundi Imalilo Nutrition Educators wamesema kupitia mikopo hiyo wameweza kuwa na mitaji ya kutosha ya kuendesha biashara zao.

Clara Sanga ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi hicho anayejishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za Lishe ameishukuru Halmshauri ya Manispaa ya Temeke kwa kuwapatia mkopo huo ambao umewainua kiuchumi na kuwawezesha kutengeneza ajira zaidi kwa vijana wengi.

“Kabla ya kupata mkopo huu nilikuwa nikisuasua katika biashara yangu na kupelekea kutokufikia malengo husika lakini baada ya kupata mkopo wa asilimia 10 kutoka Halmshauri ya Manispaa ya Temeke nimetimiza malengo yangu na biashara yangu imekuwa “amesema

Naye Teddy Minja mnufaika wa mkopo wa asilimia 10 anayejishughulisha na ufungaji wa Ngo’mbe wa maziwa amesema kabla ya kupata mkopo alikuwa anamtaji wa kutosha pamoja na masoko ya kuuza Maziwa.

Amesema baada ya kupata mkopo amekuwa akishiriki katika maonesho makubwa ikiwemo maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea ambapo ameweza kujitagaza zaidi na kupata wateja.

Aidha aliwataka wanawake wasiogope kuchukua mikopo kutoka Halmshauri na kusisitiza kuwa wakope kwa ajili kufanyia kazi ambayo wameikusudia.

Kwa upande wake Devotha Karia ambaye anajishughulisha na utegenezaji wa bidhaa za batiki amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaona wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kuamua kuwapa mikopo isiyokuwa na riba.

“Kupitia Halmshauri ya Wilaya Temeke tumeweza kunufaika na mkopo wa asilimia 10 ambao kwa kweli umeinua biashara zetu na kutukwamua kiuchumi”amesema

Aidha amewapongeza maofisa biashara wa Halmshauri ya Manispaa ya Temeke kwa kuwapa elimu pamoja na kuwatafutia masoko.

Naye Ofisa biashara kutoka Halmshauri ya Manispaa ya Temeke, Dotto Killangi amesema wanatumia maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu fursa mbalimbali zilizopo Temeke.

Amesema elimu hiyo imekuwa ikitolewa katika eneo la Viwanda pamoja na kutoa huduma ikiwemo za leseni za biashara na vibali mbalimbali.