Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Arusha
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na jeshi la polisi wilayani Karatu mkoani Arusha imewakamata watu wanne kwa tuhuma za utapeli kwa wafanyabiashara wilayani hapo.
Watu hao walikamatwa Novemba 22, mwaka huu mchana katika maeneo ya hoteli ya Manyara baada ya kupita kwenye maduka makubwa ya wafanyabiashara na kukagua mashine za kutolea risiti huku wakidai fedha.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba amesema kuwa watu hao kwa sasa wako mikononi mwa polisi kwa mahojiano walikamatwa kwa msaada wa wafanyabiashara ambao waliombwa rushwa kwa madai ya kukosea taratibu za ulipaji wa kodi.
” Taarifa tulizopata kwa baadhi ya wafanyabiashara waliopitiwa na watu hao wamesema kuwa watu hao walijitambulisha kuwa maofisa wa TRA kutoka makao makuu wakiwa na gari aina ya Prado yenye namba za usajili STK 4511 huku wakiwa wamevaa vitambulisho vyenye nembo za TRA ambapo walikuwa wakikagua risiti za wafanyabiashara na kutafuta makosa na kudai rushwa,”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Amesema kuwa baada ya wafanyabiashara kuona sura ngeni ndipo baadhi walipotoa taarifa kwa Maofisa wa TRA Karatu ambapo waliwataka wasitoe kiasi chochote cha fedha ndipo walipotoa taarifa polisi na watu hao kufuatiliwa ambapo walikamatwa wakiwa wanatoroka katika eneo la hoteli ya Manyara kwa ushirikiano wa polisi na boda boda.
Amesema baada ya kuona wanafuatiliwa walibadili namba hiyo ya gari ambapo walifika hotelini hapo kama wageni ndipo walipotiwa mbaroni na mwingine kutoroka ambapo amekamatwa siku ya pili.
Pia amewahakikishia wananchi wilayani hapo kuwa vyombo vya usalama vya wilaya viko imara muda wote ambapo aliwaasa wafanyabiashara kuhakikisha anayejitambulisha kuwa Ofisa wa TRA anakuwa na kitambulisho kinachosomeka na wasitoe nafasi ya kuwapa fedha bila Control namba za malipo ya serikali.
Kwa upande wake Ofisa wa TRA Mkoa wa Arusha Hamenyimana Njagamba amewaomba wafanyabiashara kujiamini katika biashara zao wanazozifanya na kutokuwa waoga wa risiti wanazozitoa kwani kufanya hivo ni kutoa mianya ya matapeli kupata nafasi ya kuwatapeli.
“Msikubali kutapeliwa kirahisi,akija mtu anajitambulisha yeye ni Ofisa wa TRA muulize kitambulisho,angalia jina lake na nembo ya TRA na usilipe fedha yoyote bila Contol namba,”amesema Njagamba.
Amewasihi wafanyabiashara kuwa matapeli wamekuwa wengi hivyo watoe ushirikiano kwa ofisi ya TRA au kituo cha polisi pale wanapoona kiashiria cha matapeli katika maeneo yao ya biashara
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Jastin Masejo akizungumza na vyombo vya habari alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo aliwataka wananchi kujihadhari na matapeli katika maeneo yao na kuwahakikishia kuwa vyombo vya usalama viko imara.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa