November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanazuoni LGTI washauri serikali kushughulikia mapungufu uchaguzi serikali za mitaa 2024

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

CHUO cha Serikali za Mitaa(LGTI)Hombolo,kupitia wanazuoni pamoja na wataalamu wa chuo hicho wameishauri serikali kufanyiakazi mapungufu mbalimbali ikiwemo ushiriki mdogo wa wanawake na watu wenye ulemavu katika kugombea nafasi za uongozi ili kupata viongozi bora kwa maslahi ya Taifa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo na Naibu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma,Utafiti na ushauri wa Chuo cha Serikali za mitaa,Dkt.Michael Msendekwa wakati wa Kongamano la 15 la wanazuoni ambapo alisema mada hiyo inatoa dira na muelekeo wa uchaguzi ujao wa serikali za mitaa mwaka 2024.

“Leo tumekuwa na Kongamano la 15 la wanazuoni ambapo pamoja na kuongelea mambo mengi lakini kubwa ni kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii nchini ,

“Tumekuja na mada hii kutokana tafiti zilizofanywa na wanazuoni zinaonesha Wanawake hawashiriki katika kama wachaguliwa bali wanachagua hivyo tumejadili ni jinsi gani wanawake wanaweza wakashiriki katika uchaguzi huo kwasababu imeonekana kuwa ushiriki wao ni mdogo hususani kwenye kupigiwa kura,”amesema Dkt.Msendekwa.

Hatahivyo amesema mada hiyo inaenda mbali zaidi kwani walijadilo ni jinsi gani watu au uchaguzi wa viongozi ambao unaweza ukachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ambapo amesema wanazuoni wameona kwamba wakichaguliwa viongozi wazuri katika mamlaka za serikali za mtaa watakuwa ni kichocheo kizuri katika kuleta maendeleo na mandeleo ya kiuchumi lakini maendeleo ya kijamii kwani wakipatikana viongozi wazuri kutakuwa na watu wenye afya nzuri na waliokua kimandeleo.

“Maana yake hawatataka rushwa wala kitu chochote kwasababu tayari wao wenyewe wameendelea kiuchumi na kijamii kwahiyo hizi mada zitatusaidia sana sana katika kujboresha au kama kichocheo kikubwa katika uchaguzi wetu wa serikali za mitaa 2024 hivyo tunashukuru na kuishauri serikali ichukue haya maoni yetu mapendekezo ya wanazuoni ambayo wameyajadili ili wayafanyie kazi kwasababu maoni na mapendekezo haya yamejikita sana katika utafiti kwahiyo mambo ambayo yalikuwa yanaongelwa tumefanya tafiti katika mambo mengi ya maendeleo,”amesema Dkt.Msendekwa.

Ameeleza kuwa wanataka maamuzi ya serikali yawe yanatokana na tafiti mbalimbali kwani tafiti hizo zinatoa majibu au taarifa ya vitugani tunatakiwa kufanya kwahiyo ni mada ambazo zimetokana na tafiti mbalimbali.

” Kwahiyo tutazitengeneza na kuzipeleka serikalini na kushautu kuwa haya mapendekezo yanatokana na tafiti mbalimbali na yakizingatiwa hayo tutaboresha uchaguzi wetu na tukiboresha uchaguzi wetu tatapata maendeleo ambayo tunakusudia ya maendeleo ya kiuchumi,kijamii na kisiasa nchini,”amesema Dkt.Msendekwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo LGTI
Mashala Lameck,alisema kuwa kongamano hilo la wanataaluma ambalo linafanyika siku moja kabla ya mahafali kwa kila mwaka na wao wamechagua ya mada uchaguzi wa serikali za mtaa na kwamba wanaangalia mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa watanzania.

“Mada hii ni nzuri kwa maana inatupa muelekeo tunavyoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwakani,utupe sasa mawazo kupitia wanataaluma ambayo yataisaidia sasa serikali katika kuboresha uchaguzi huo kwahiyo kongamano la leo lina aksi kabisa tukio la mwakani la kupata viongozi katika ngazi za msingi za mamlaka za serikali za mitaa kwahiyo itachangia katika kushuari sisi kama watafiti wana taaluma kuishauri serikali maboresho yatakayofanyika ili uchaguzi wa serikali za mitaa uwe na tija mwakani,

“Tulisukumwa kuja na mada hii mwaka huu kwasababu sisi ni chuo cha serikali za mitaa kwahiyo eneo letu sisi ni kuishauri serikali kupitia tafiti,kupitia mafunzo lakini kupitia ushauri wa kitaalamu kwahiyo tumekuja na mada hii mapema kwasababu tukijua tukio la mwakani linatuhusu sisi kama chuo,kwamba chuo tufanye maandalizi mapema kabla ya uchaguzi huo tukiamini kabisa uchagzi utafanyika kabla ya kongamano jingine la wanataaluma la hapo mwakani kwasbabu tunaamini mahafali yanafanyika mwezi Disemba na uchaguzi unafanyika mwezi wa Oktoba,

“Kwahiyo Kongamano hili linatusaidia sasa ili mwakani na sisi tuweze kuweka sawa mifumo yetu lakini pia tuweze kuishauri namna bora serikali kupitia TAMISEMI namna itakavyoweza kuliendesha zoezi hili.

Naye Rais wa Kongamano hilo , Suma Mwampulo amesema mada hiyo inawawezesha kuweza kudadavua zaidi masuala ya uchaguzi na uendeshaji wake lakini pia kutoa elimu kwa wapiga kura watarajiwa ,ikiwa wanafunzi ni wapiga kura watarijiwa kuhamasisha vijana kushiriki katika zoezi la uchaguzi lakini pia wawe sehemu ya kutoa elimu katika jamii umuhimu wa kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Akizungumza katika Kongamano hilo mgeni rasmi kuyoka Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Sospeter Mtwale alisema kuwa amesikiliza mada katika Kongamano hilo la wanazuoni kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na wao kama serikali wameyachukua na kuyapokea na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi kuyafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu na kanuni za serikali .

“Kwa maana uchaguzi maendeleo ya jamii pamoja na maendeleo ya kiuchumi kwa hiyo uchaguzi huo unafanyika mwakani kwahiyo Kongamano hilo lilikuwa ljnatoa muelekeo na dira kuona namna gani sisi kama serikali tunaweza kujipanga kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu,

“Yametolewa maoni mbalimbali na wanazuoni wabobevu pamoja na wanafunzi wa chuo hiki hivyo nitoe wito kwa chuo chetu cha Hombolo kiendelee kufanya makongamano mengi kama haya kuhakikisha wanaisaidia Ofisi ya Rais TAMISEMI kama serikali inasimamia Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa ili basi maendeleo yaende kwa wananchi tuweze kuleta maendeleo kwa wananchi wote,”amesema Mtwale.