Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Upasuaji wa bure wa urekebishaji wa viungo umefanikiwa kuwasaidia Watanzania 16 wenye ulemavu na majeraha yaliyotokana na ukatili, ajali na moto, waliopatiwa huduma hiyo hivi karibuni.
Akieleza umuhimu wa kambi hiyo, hapo jana, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya, Dk. Hamad Nyembea amesema huduma hiyo inaokoa maisha ya wengi na kuirejeshea jamii nguvu kazi, huku akiipongeza Hospitali ya Aga Khan kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya afya.
Amesema miaka kumi iliyopita kulikuwa na uhaba wa wataalamu wa upasuaji rekebishi, lakini kwa sasa idadi inaongezeka huku wengine wakiendelea kusomea taaluma hiyo, hatua aliyoitaja kuwa ni mafanikio muhimu. Kutokana na mafanikio ya kambi hiyo, Dk. Nyembea amesema atapendekeza ifanyike mara mbili kwa mwaka ili kuongeza idadi ya wanufaika.
Kwa mujibu wake, zaidi ya watu 300 tayari wamenufaika na huduma hiyo tangu ilipoanza nchini. Ameongeza kuwa ujio wa madaktari bingwa kutoka nje umechangia kuanzishwa kwa idara maalum katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambayo sasa ina wataalamu bingwa 13 wa upasuaji rekebishi.
Serikali kwa kushirikiana na Hospitali ya Aga Khan imefanikiwa kuanzisha huduma hiyo iliyoanzia Muhimbili na sasa inaendelea kusambazwa katika hospitali nyingine nchini. Hata hivyo, amesema changamoto bado ni kubwa na wanufaika wengi wanatoka Dar es Salaam, hivyo juhudi zinafanyika kuhamasisha wananchi kutoka maeneo mengine kujitokeza zaidi.
Daktari Bingwa wa Upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan, Dk. Aidan Njau amesema programu hiyo inalenga kuwasaidia hasa wanawake waliopata madhara ya kiafya kutokana na ajali, moto na saratani. Ameongeza kuwa zoezi hilo pia hutoa fursa ya kubadilishana ujuzi kati ya wataalamu wa ndani na wale kutoka Marekani na Ulaya, pamoja na kuwajengea uwezo wanafunzi wa udaktari kupitia teknolojia mpya.
Amesema mpango huo, unaoendeshwa kwa zaidi ya miaka 10 sasa, hutolewa bila malipo kwa msaada wa washirika wa ndani na nje ya nchi. Kila mwaka, Watanzania wengi hupata majeraha ya moto, ulemavu wa kuzaliwa au ajali, hali inayoweza kusababisha ulemavu wa kudumu iwapo haitatibiwa kwa wakati. Kupitia mpango huu, wagonjwa hupata fursa ya pili ya maisha.
Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Urekebishaji na Plastiki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Edwin Mrema amesema zaidi ya wagonjwa 264 wamenufaika na huduma hiyo kupitia ushirikiano huo. Aidha, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeanzisha mafunzo ya upasuaji rekebishi tangu mwaka 2019 ili kuzalisha wataalamu zaidi wa ndani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni za Kliniki wa Hospitali ya Aga Khan, Dkt. Murtaza Mukhtar amesema gharama za kambi hiyo ni kubwa, hivyo wanashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Stanbic Tanzania, ambayo imetoa zaidi ya shilingi milioni 45 kufanikisha zoezi hilo.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT