Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
WANAWAKE na vijana 16 Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wameanza kunufaika na Program maalumu ya Imbeju baada ya kuwezeshwa mtaji wa kiasi cha milioni 15 kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha tangawizi Kata ya Lewa, Tarafa ya Bungu.
Program ya Imbeju iliyoanzishwa CRDB Foundation, lengo kubwa likiwa ni kuwainua vijana na wanawake ambao wanashindwa kujiendeleza kwa sababu ya kukosa mtaji ambayo imefika kwenye kata za Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Korogwe Ronald Paul kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wakati alipopewa nafasi ya kueleza shughuli za benki hiyo ikiwemo mikopo kwa watumishi, wakulima, wajasiriamali na makundi maalumu.
“Nia yetu ni kuona wanawake na vijana wanajikwamua kiuchumi pia tunatoa mikopo kwa watumishi, wakulima hasa wa mkonge, wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa, na wafanyabiashara wengine, ambapo mkopo kwa wajasiriamali wanakopeshwa kuanzia milioni moja hadi bilioni mbili,”amesema Paul.
“Benki ya CRDB pia inatoa mikopo kwa watumishi ili apate mkopo, sio lazima mshahara wake upitie kwenye benki yetu bali tunahitaji barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Utumishi, ambapo mikopo yetu inawalenga watumushi wote hasa walimu kwenye shule za msingi na sekondari, afya na kilimo,” amesema Paul.
Kwa watumishi wana uwezo wa kukopa hadi milioni milioni 200 na marejesho hadi miaka tisa kwa watumishi wa serikali ambayo
riba yake ni kuanzia asilimia 13 na itategemea na mshahara wake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mratibu wa Imbeju, Benki ya CRDB Tawi la Korogwe Lucy Chuwa, amesema muitikio wa wanawake na vijana kutaka kupata mikopo kupitia programu hiyo ni mkubwa,tayari wamefika kwenye vijiji vya kata za Lewa, Mpale, Lutindi, Dindira, Bungu, Mgwashi na Milungui katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
“Pia tumekwenda kwenye kata za Halmashauri ya Bumbuli ikiwemo Kata ya Mgwashi Tumekuwa tunawaeleza faida za kuweza kuendeleza shughuli zao za kiuchumi kupitia mikopo ya Imbeju ili waweze kujikwamua kimaisha na muitikio ni mkubwa,”.
Pia amesema kuwa wanatoa mtaji wezeshi kuanzia 200,000 mpaka 5,000,000 ambao unarejeshwa ndani ya mwaka mmoja, na gharama za uendeshaji ni asilimia saba.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024