Na Martha Fatael
Jamii ya watu wenye ulemavu mkoani Kilimanjaro, hususani wanawake wenye ulemavu wa uti wa mgongo,wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma bora za afya ya uzazi.Hali wanayoieleza kuwa inatishia usalama wa maisha yao wakati wa ujauzito na kujifungua.
Awali wakizungumza na mwandishi wa makala haya,baadhi ya wanawake wanasema,wanajikuta wakiishi kwa hofu ya kubeba ujauzito kutokana na changamoto wanazokutana nazo hospitalini na kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
“Wakati mwingine unaona bora usizae kabisa kwa sababu huduma hospitalini si rafiki kwetu,”anasema Anna Msekela
Huku Sara Hingu, anasisitiza,“ukifika hospitalini, wauguzi wengine wanashindwa hata kujua jinsi ya kutuhudumia kwa usahihi,”.
Wanawake hawa,wanasema hata bima za afya wanazozimiliki mara nyingi hushindwa kugharamia vifaa maalum vinavyohitajika na watu wenye ulemavu, kama vile catheter, nepi za watu wazima, au dawa za kuzuia maambukizi ya mfumo wa mkojo.
Aidha, gharama za usafiri kutoka nyumbani hadi hospitalini zimekuwa mzigo hasa kwa wale wanaotumia viti mwendo na kuhitaji usafiri maalum.
“Unaweza kuambiwa kituo kiko karibu, lakini kwa sisi wenye ulemavu, ‘karibu’ ni mbali sana kwa sababu hakuna njia rafiki za kutufikisha huko,”anasema Sara Hingu.
Unyanyapaa na uelewa mdogo
Wanaeleza pia kuwa changamoto kubwa zaidi ni unyanyapaa kutoka kwa baadhi ya wahudumu na wananchi.
“Wengine wanashangaa mtu mwenye ulemavu kuwa na ujauzito.Wengine hata wanakuuliza ‘uliwezaje kubeba mimba?’ maneno ya aina hiyo yanaumiza sana,” anasema Anna Msekela.
Sheria zipo,utekelezaji mdogo
Licha ya kuwepo kwa sheria na sera zinazolinda haki za wenye ulemavu, bado kuna pengo kubwa kati ya maandiko ya kisheria na utekelezaji wake katika vituo vya afya.
Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010, kifungu cha 26, inaitaka serikali kuhakikisha kuna kuwa na huduma za afya, ustawi na vifaa tiba vinavyokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Huku Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 11(1), inatamka kuwa serikali ina wajibu wa kutunza ustawi wa wananchi wake wote, wakiwemo wenye ulemavu, wakati wa ugonjwa au uzee hata hivyo, hali halisi inaonesha changamoto zipo nyingi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Uti wa Mgongo (KASI) Mkoa wa Kilimanjaro, Stella Maimu, anasema wanawake wenye ulemavu hukumbana na vikwazo maradufu wanapohitaji huduma za uzazi.
“Mama mwenye ulemavu akitaka kujifungua anakumbana na mateso mara mbili. Kwanza, kufika hospitalini ni changamoto kutokana na miundombinu isiyo rafiki; pili, vitanda vingi vya uzazi havimpi uwezo wa kujihudumia mwenyewe,” anasema Maimu.
Maimu, anasema, upungufu wa wataalamu wa afya waliobobea kuhudumia watu wenye ulemavu pia ni tatizo.
“Kuna mama mmoja katika chama chetu alifariki wakati wa kujifungua, si kwa sababu huduma hazikuwepo, bali kwa sababu hakupata mtaalamu aliyemwelewa vizuri,”anasema Maimu.
Hali ya uchumi pia ni kikwazo
Maimu, anasema hali ya kiuchumi huongeza mzigo kwa wanawake wenye ulemavu.
“Tunahitaji vifaa maalum kama mpira wa kutolea haja ndogo (catheter) unaogharimu zaidi ya shilingi 6,000 kila wiki.Ukikosa, unaweza kupata maambukizi.Wengine tunahitaji nepi, lakini gharama ni kubwa,”anasema.
Pia watu wenye ulemavu wa miguu, mikono, uoni hafifu na usikivu pia hukumbana na changamoto zinazofanana.
Wengi wao hukosa taarifa sahihi za afya ya uzazi kutokana na ukosefu wa wahudumu wenye uelewa wa mawasiliano kwa njia ya alama, maandishi makubwa au vifaa saidizi kama viti mwendo na lifti hospitalini.
Tafiti na takwimu
Tafiti zinaonesha kuwa hali hii si ya Moshi pekee kwani kwa mujibu wa utafiti wa UNFPA Tanzania (2022) unaonesha kuwa asilimia 11.03 ya Watanzania wazima wana ulemavu wa aina mbalimbali, wanawake wakiwa asilimia 11.9 ikilinganishwa na wanaume asilimia 10.
Hata hivyo, zaidi ya nusu ya wanawake hao hawapati huduma za uzazi salama kutokana na ukosefu wa vifaa, miundombinu rafiki na uelewa mdogo wa wahudumu.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), watu wenye ulemavu nchini ni takribani milioni 3.6, sawa na asilimia 11.3 ya Watanzania wote.
Takwimu hizi zinaonesha ukubwa wa kundi hili ambalo bado halijapewa kipaumbele cha kutosha katika huduma za afya ya uzazi.
DMO Moshi anena
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Moshi (DMO), Dkt. Juma Mombokaleo, anakiri changamoto kuwepo kwa changamoto hizo.
“Ni kweli bado hatuna vituo maalum wala wataalamu wa kudumu kwa ajili ya kundi hili. Tunatoa mafunzo kwa wahudumu wetu pale fursa zinapopatikana, kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kama CCBRT na Faraja Forward,” anasema Dkt. Mombokaleo.
Mashirika hayo yameanzisha programu katika zaidi ya vituo 30 vya afya wilayani humo, zikilenga kutoa elimu ya afya ya uzazi, kuwafichua watu wenye ulemavu wanaofichwa nyumbani na kutoa vifaa tiba vinavyosaidia kuongeza usalama wakati wa ujauzito na kujifungua.
Hata hivyo, changamoto ya miundombinu isiyo rafiki bado inaendelea ambapo Mkuu wa Idara ya Physiotherapy na Occupational Therapy katika kituo cha CCBRT Moshi, Sabasi Kimario, anasema wanashirikiana na serikali kutoa matibabu na elimu ya afya ya uzazi salama kwa wanawake wenye ulemavu.
“Tunamsaidia mama aliyepata ajali na kuumia uti wa mgongo kuendelea na maisha. Pia tunatoa huduma za upasuaji wa fistula na urejeshaji wa viungo,” anasema Kimario.
Kimario anafafanua kuwa CCBRT inahusisha huduma za tiba ya viungo, ushauri wa kisaikolojia, uhamasishaji wa haki za uzazi salama pamoja na mafunzo kwa wahudumu wa afya kuhusu namna bora ya kuwahudumia watu wenye ulemavu.
“Tunatoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga kuhusu namna ya kuwahudumia wateja wanaotumia viti mwendo, hasa katika mazingira ya uzazi. Pia tunashirikiana na hospitali za serikali kuhakikisha vifaa vinavyotolewa vinakidhi mahitaji ya makundi maalum,” anaeleza.
Aidha, anasema kituo hicho kimekuwa kikifanya ufuatiliaji wa kina kwa wanawake wenye ulemavu baada ya kujifungua ili kuhakikisha wanapata usaidizi wa tiba ya viungo na ushauri wa lishe.
“Hii inasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na matatizo ya baada ya kujifungua.Ninaiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuingiza vifaa tiba kwenye bima ili kuwasaidia zaidi watu wenye ulemavu maana gharama zake ni kubwa na wanahitajika kulipa kwa fedha taslimu na wengi hushindwa kumudu,” anasema Kimario.
Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Taifa (2007), serikali ina wajibu wa kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa usawa bila ubaguzi.
Sera ya Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu (2004) inasisitiza pia umuhimu wa huduma rafiki za afya kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo huduma za uzazi.
Sanjari na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2025–2030, Ibara ya 110, inaeleza dhamira ya serikali,kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wote bila ubaguzi, wakiwemo watu wenye ulemavu na makundi maalum ya kijamii.
Hata hivyo, utekelezaji katika ngazi za Halmashauri bado unakwamishwa na bajeti ndogo, ukosefu wa takwimu maalum, na upungufu wa wataalamu waliobobea katika afya ya uzazi kwa watu wenye ulemavu.
Licha ya jitihada ndogo zinazoendelea, hali ya wanawake wenye ulemavu wilayani Moshi bado inaonesha pengo kubwa kati ya sera na uhalisia. Wengi wao hawapati huduma za uzazi salama, elimu ya afya, wala mazingira rafiki hospitalini.
Mashirika kama KASI, CCBRT, na Tusonge yameendelea kutoa elimu na usaidizi, lakini suluhisho la kudumu linahitaji ushirikiano mpana zaidi wa serikali, jamii na wanasiasa.Kama Katiba na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu zinavyotamka, upatikanaji wa huduma bora za afya ni haki ya msingi si hisani.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama