Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mkurugenzi Idara ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Makundi Maalumu(SMT) ndugu Badru Abdulnuru amewataka wajasiriamali wanawake kutumia vyema fursa ya mikopo ili kuendelea biashara zao.
Akizungumza wakati alipofungua mafunzo kwa wajasiriamali hao juu ya namna ya kuomba mikopo isiyo na riba katika Benki ya CRDB, yaliyofanyika jana katika ukumnbi wa Sebleni kwa wazee ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha siku ya wanawake duniani, ndugu badru amesema kufanya hivyo kutawasaidia kuweza kujikwamua na utegemezi.
Amewataka wanawake hao kutambua kuwa katika mikopo hio ya CRDB Serikali nayo imechangia kwa kiasi kikubwa ili kuwasaidia wanawake kuwainua kiuchumi.
Pia amewataka kuwa na nidhamu ya fedha wanazikopa kwa kufanya jambo walilolikusudia ili waweze kurejesha mikopo hiyo na kuwasaidia wengine.
Aidha amewashauri kuyatumia majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi ili kuweza kuwakutanisha na wajasiriamali wengine Pamoja na kutanua wigo wa kibishara.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto (SMZ) bi Siti Abass Ali amesema Wanawake nchini wametakiwa kujitathmini na kujitambua katika kupambana katika kujiletea maendeleo wenyewe.
Mkurugenzi Siti ameyasema hayo, wakati alipofungua mafunzo ya wajasiriamali kwa wanawake wa wilaya mbalimbali za Unguja, ikiiwa ni shamrashamra za kuadhimisha siku ya wanawake duniani Machi,08.
Amesema wanapoadhimisha siku ya wanawake duniani kila mwaka nilazima wanawake kujitathmini katika mwaka mzima ni kitu gani wamefanya katika kujiletea maendeleo na endapo kuna tatizo ni vyema kulitatua ili kusonga mbele kimaisha.
Amesema Wizara imeamua kufanya mafunzo kwa wajasiriamali wanawake, ikiwa lengo ni kuwaunganisha pamoja wanawake na kupeana moyo katika maendeleo, pamoja na kupeana nguvu kwa kugombania nafasi mbalimbali za uongozi ili kuweza kuwa mbele kimaendeleo.
Kwa upende wao baadhi ya wajasiriamali hao, wameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa kuweza kuwapatia elimu hiyo ambapo wameomba kusaidiwa katika kupunguziwa masharti ya upatikanaji wa mikopo ili nao waweze kunufaika.
Pia wamewaomba wafadhili wanapotoa misaada mbalimbali kwa wajasiriamali kufika vijijini kwani wamedai kuwa fursa hizo wamekuwa wakizikosa ukilinganisha na watu wanaoishi mjini.
Mafunzo hayo ya siku mbili kwa wajasiriamali wanawake yamefanyika katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkoa wa Kaskazini, na Mkoa wa Kusini, ambapo maada mbalimbali ziimewasilishwa ikiwemo matumizi sahihi ya fedha, nafasi za uongozi kwa wanwake na nyenginezo.
More Stories
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali