Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online
MFUKO wa huduma.za Fedha (SELF Microfinance Fund ) umesema imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 43 kwa wanufaika zaidi ya 38,000 nchini katika mwaka 2025, huku wanawake wakichangia zaidi ya asilimia 51 ya wanufaika wote.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Masoko wa SELF MF, Petro Mattaba, wakati akielezea huduma zinazotolewa na taasisi hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.
Mattaba alisema SELF MF, ambayo ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha, inaendelea kutekeleza jukumu la kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo, huduma za bima na elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ya jamii.
Alisema huduma za mikopo zinawalenga watumishi wa umma, wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakulima, wafugaji na wavuvi, huku sehemu nyingine ya mikopo ikitolewa kupitia taasisi za huduma ndogo za fedha ili kuwafikia wananchi waliopo katika maeneo ambayo mfuko hauwezi kuyahudumia moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Mattaba, SELF MF ina matawi 12 Tanzania Bara na tawi moja Zanzibar, hatua inayorahisisha wananchi kupata huduma za kifedha pamoja na ushauri wa matumizi sahihi ya fedha.
Alieleza kuwa taasisi hiyo inaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan vijana, wanawake na makundi mengine maalumu kupitia mikopo yenye masharti nafuu.
Wakati huo huo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipotembelea banda la SELF MF katika maonesho hayo, alipata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo pamoja na mchango wake katika kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kuongeza fursa za upatikanaji wa mitaji kwa wananchi nchini.

More Stories
TOSCI Yahimiza Matumizi ya Mbegu Zilizohakikiwa
Waziri apongeza NBS kuweka Takwimu Mtandaoni
Waziri Kapinga apongeza mafanikio ya TTCL