Na Happiness Bagambi
TANZANIA inatajwa kuwa ya kwanza barani Afrika kufanikiwa kusambaza umeme maeneo mengi nchini kwa takribani asilimia 80.
Kazi ya kusambaza umeme nchini kwa kiasi kikubwa imefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.
Hiyo inathibitishwa na kauli ya Rais Magufuli anapohutubia mikutano yake ya kampeni ambapo hivi sasa vimebaki zaidi ya 2000 umeme kufika vijiji vyote.
Mfano, mkoani Kagera, Rais Magufuli alisema alipokuwa akiingia madarakani mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa na umeme ni 168, lakini vimeongezeka hadi kufikia vijiji 541 na ambavyo vimebaki havina umeme ni 123 .
Anaahidi kuwa endapoo akichaguliwa tena ndani ya miaka mitatu ya mwanzo vijiji ambavyo vimebakia katika mkoa huo havina umeme vitakuwa na umeme.
“Tanzania itakua na umeme wa kutosha na hasa baada ya kukamilika bwawa la Julius Nyerere ambalo litakuwa linazalishaa megawati 2115,”alisema.
Mkakati wa Serikali kusambaza umeme nchi nzima una dhamira ya kubadilisha maisha ya Watanzania, hasa wanawake. Leo hii mwananchi wa kawaida hasa mwanamke wa hadi leo hii bado wanaendelea kutumia mkaa na kuni katika matumizi yake ya kupika kila siku.
Hii inaonesha jinsi gani nchi zetu za Kiafrika zilivyobaki nyuma kimaendeleo, kwani mataifa yaliyoendelea yana uhakika wa kutumia nishati ya umeme na gesi katika matumizi yake yote ya kila siku, hatua ambayo Serikali imedhamiria kutufikisha.
Hiyo ni kwa sababu Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya rasilimali ya nishati, ikiwemo gesi asilia, maporomoko ya maji, upepo, makaa ya mawe nk.
Aidha, nchi yetu ni kati ya nchi zinazotekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 ambapo moja ya malengo hayo ni kuhakikisha wananchi wake wanapata nishati bora na kwa bei nafuu kwa matumizi yao ya kila siku nyumbani kama kupikia badala ya kuendelea kukata miti kwa ajili ya kupata mkaa na kuni, ili kuepuka uharibifu wa mazingira.
Kwa msingi huo hatuna budi kuishukuru Wizara ya Nishati chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano kwa uwajibikaji wake, kwani Tanzania kushika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kusambaza umeme nchini kote si jambo rahisi hasa kutokana na changamoto zilizopo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hivi karibuni wakati akieleza mafanikio ya Serikali kwenye mkutano wa viongozi wa dini wa kamati za amani za mikoa mbalimbali nchini uliofanyika katika kituo cha mikutano cha mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, alisema hadi April 2020 vijiji 9,112 vilikuwa vimefikiwa na umeme hapa nchini.
Pamoja na Tanzania kuwa ya kwanza kwa kuwapelekea wananchi wake umeme hadi vijijini kwa ajili ya matumizi yao, lakini bado wananchi wa kawaida hasa wanawake hawajanufaika na nishati hii, kwani wanaendelea kutumia kuni na mkaa kila siku.
Nchi yetu ikipataumeme wa kutoshsa itaondokana na Matumizi ya kuni na mkaa yanayochangia kuendelea kuwepo uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ili kutengeneza mkaa.
Nishati ya umeme ni muhimu Katika jamii, hasa kwa mwanamke ambaye ndiye nguzo ya kuhakikisha familia inakula chakula bora na kilichopikwa, kwani wanaume wao hubaki wanamtegemea mwanamke huyo huyo.
Wanaume wanataka wakirudi nyumbani wakute mwanamke chakula kimeiva na hawana haja ya kujua kimepikwa kwa mkaa, kuni, umeme au gesi? Wao wanataka wakute kimeiva wapakuliwe wale pamoja na watoto.
Hivyo basi pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata hapa nchini katika sekta ya nishati ya umeme, tunatarajia mwanamke pia awe wa kwanza kunufaika na nishati hii au gesi kwa matumizi yake ya kila siku ili kuondokana na gharama za kununua mkaa unaotokana na ukataji miti na kuharibu mazingira, kwani mwanamke ndiye anakumbwa moja kwa moja na maisha ya familia.
Aidha, gunia la mkaa linanunuliwa kati ya sh 50,000 hadi 75,000, ambalo halitoshi kwa matumizi ya mwezi kwa familia ya watu watano. Kwa upande wa kuni vipande vitatu ni kati ya sh. 3,000 hadi 5,000 kwa siku, gharama ambazo haziendani na hali ya maisha ya mwananchi hasa mwanamke wa hali ya kawaida.
Kwa msingi huo bado hatujafikia lile lengo la umeme bora na wa uhakika na wenye bei nafuu kwa kila Mtanzania. Tanzania tunahitaji nishati ya umeme ambao utamuondolea mwanamke adha na makali ya maisha ya kila siku na kumpunguzia gharama ya manunuzi pamoja na kuondoa uharibifu wa mazingira endapo kila mwananchi atapika chakula chake kwa kutumia umeme au gesi.
Kimsingi huu umeme uliopo bado haujamsaidia mwananchi kuupikia pale anapohitaji.
Aidha bado wanahitajika wataalamu kuelimisha jamii iondokane na dhana ya matumizi ya mkaa na kuni. Elimu hiyo itasaidia wananchi kuacha kukata miti, kwani rasilimali hizi ni mali asili inayolinda ardhi na kuleta mvua.
Mara nyingi changamoto hizi kwa mwanamke huwa haziangaliwi kwa mapana kutokana na kuwa hazionekani ukubwa wake kwa macho, lakini kiuhalisia zinamtesa mwanamke ambaye ndiye muhimili mkubwa katika maisha ya familia.
Aidha bado zinahitajika hatua za makusudi za kuwaelimisha wananchi kuhusiana na matumizi mbalimba ya umeme ili wasiishie kuutumia kwa ajili ya taa za nyumbani.
Hatua ya kusambaza umeme iende sambaamba na Serikali kuwezesha familia na jamii kujivunia umeme na gesi kwa matumizi yote ya nyumbani.
Tanzania inahitaji uchumi wa viwanda kwa ajili ya maendeleo ya nchi, lakini pia haya yaanzie katika familia ili iwe na uhakika wa kutumia nishati ya umeme wakati wote hasa katika mapishi ya kila siku ili kuondoa changamoto kwa mwanamke.
Endapo wakianza kutumia umeme kwa matumizi sahihi ikiwemo kupikia itawasaidia zaidi kujua kazi nzuri na matunda mazuri yaliyoletwa na uongozi wa awamu ya tano.
Katika jitahada hizi kubwa tutafikia malengo endapo tutashirikiana na wadau mbalimbali wa nishati wa ndani na nje ya nchi ili kupunguza changamoto zilizopo ikiwemo; upungufu wa fedha za kutosha, ushiriki na uwekezaji mdogo wa sekta binafsi katika miradi mikubwa ya nishati na utegemezi katika chanzo cha nishati, gharama kubwa za tozo za uhunganishaji na usambazaji umeme, upungufu wa wataalamu na tafiti katika sekta ya hiyo.
Katika kutekeleza hayo, Serikali kupitia TANESCO Tanzania, imeamua kutumia wataalamu wa ndani ya nchi ili kupunguza gharama katika kutekeleza na kusimamia miradi mikubwa na ya kimkakati ambapo hiyo itasaidia kumpunguzia mwananchi gharama za tozo ya umeme hapa nchini.
Tanzania inaonesha kuwa, nishati jadidifu zisizo za maporomoko ya maji zinajumuishwa kwa asilimia tatu tu katika mchanganyiko wa nishati nchini ifikapo mwaka 2035 (Policy Forum)
Serikali pia ikusudie kuongeza vivutio vya uwekezaji wa sekta binafsi hasa katika miradi mikubwa ya nishati ili kupunguza kuendelea kutegemea misaada kutoka kwa wahisani na mikopo kutoka katika taasisi za kifedha hali ambayo itasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania
Kwa kushirikiana na taasisi za kiraia, Serikali ifanye tafiti za maeneo ya kuwekeza katika nishati na kuweka vivutio ili kupata wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi katika nishati badala ya kupata misaada ambayo hata hivyo haitoshelezi matakwa, kwani wastani wa utoaji fedha kwa mwaka 2010/11-2016/17 ilikuwa ni chini ya asilimia 20 kwa mujibu wa ripoti ya uchambuzzi wa bajeti ya wizara iliyotolewa mwaka 2017/2018.
Aidha, naushukuru uongozi wa Serikali awamu ya tano ambao umezindua mradi wa Kinyerezi II Megawati 240 uliobuniwa ili kuongeza uwezo wa kufua umeme kutokana na gesi asilia na hivyo kuimarisha na kuongeza uwezo wa gridi ya Taifa katika kusafirisha na kusambaza umeme nchini ulioanza kazi Machi 1, 2016.
Mbali na miradi mingi iliyoanzisha, leo tunajivunia kuwa na Serikali ambayo imetekeleza ndoto za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuanzisha mradi wa umeme wa Julius Nyerere.
Tanzania inaweza kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 kama tutafanya kazi kwa kushirikiana na kuziunga mkono juhudi za serikali.
More Stories
Ushiriki wa watoto, vijana katika vita ya mabadiliko ya tabianchi
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini