Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
WANAWAKE wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga wamemlilia Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge kuwa wanawake wanatelekeza familia zao na kufanya watoto kukosa huduma ya chakula sababu ya kukimbia madeni ya mikopo kausha damu.
Na hali hiyo imekuwa mbaya zaidi baada ya Serikali kusitisha mikopo ya asilimia kumi inayotokana na Mapato ya Ndani ya Halmashauri, ambapo wanawake walikuwa wanakopeshwa asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili.
Akitoa taarifa kwa Mbunge Mhandisi Ulenge Julai 25, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kilichofanyika Ukumbi wa Maktaba Chuo cha Ualimu Korogwe, Katibu wa UWT Wilaya ya Korogwe Mjini Suzana Mandia alisema hata ndoa zinavunjika sababu ya mikopo hiyo.
“Mikopo ya kausha damu inawadhalilisha wanawake wengi wa Korogwe wanatelekeza familia zao, watoto wanateseka kwa kukosa huduma za chakula kwa wakati, ndoa zinavunjika na wanawake wanatoroka nyumba zao,tunaomba Mbunge Mhandisi Ulenge utusaidie kulifikisha hili jambo, na ikiwezekana mikopo hiyo ipigwe marufuku” amesema Mandia.
Akizungumza na wanawake hao, Mhandisi Ulenge alisema Serikali
imerejesha mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, lakini kwa kupitia benki. Na Serikali imechagua halmashauri 10 kama za majaribio nchini, ambapo kwa Mkoa wa Tanga imechaguliwa Halmashauri ya Bumbuli.
Mhandisi amesema ili wanawake kuondokana na adha hiyo, wanatakiwa kuchukua mitaji wezeshi kupitia programu ya Imbeju kutoka Benki ya CRDB, kwani mikopo yake haina riba na wanawakopesha wanawake na vijana dhamana yao ikiwa ni vikundi.
Ofisa wa Benki ya CRDB Tawi la Korogwe Lucy Chuwa, ambaye alialikwa na Mhandisi Ulenge kuzungumza na wanawake hao, amesema program ya Imbeju imeanzishwa na benki hiyo ili kuwaondolea adha wanawake na vijana katika kupata mitaji wezeshi, ambapo wanachangia asilimia saba ya mtaji huo kama gharama za uendeshaji, ambayo inawasaidia kupata mtaji na kufanya shughuli zao.
Akiwa Shule ya Sekondari Mgombezi iliyopo Halmashauri ya Mji Korogwe, Mhandisi Ulenge amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepeleka fedha nyingi za kujenga miundombinu ya shule, hivyo anatamani miundombinu hiyo iende sambamba na ufaulu kwa wanafunzi kwa kufanya vizuri kwenye masomo yao.
“Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga miundombinu bora ya elimu na Mkuu wa Shule amezungumza kwenye taarifa yake fedha zilizoletwa Mgombezi kwa ajili ya elimu,Katika mipango iliyokuwepo ya kuhakikisha shule inakuwa na kidato cha tano na sita, mimi natamani miundombinu bora iliyoletwa na Dkt. Samia iweze kuleta tija iliyo bora zaidi katika elimu mkoa wetu wa Tanga.
“Majengo yaliyoletwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan yanaweza kuwa sawa na mapambo tu iwapo hatutawekeza juhudi za makusudi kuhakikisha tunaongeza ufaulu katika shule zetu,kwahiyo watoto wangu wapendwa nimekuja kwenu leo ili kuwatia moyo katika suala zima la elimu,niliyesimama mbele yenu kitaaluma ni Mhandisi, na ili iweze kuwa Mhandisi ni lazima uwe umefaulu vizuri masomo ya kemia, fizikia na hisabati” amesema Mhandisi Ulenge.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam