Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Pemba
NGOME ya Wanawake ya Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar, imemuahidi mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ushindi mkubwa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akizungumza katika mkutano wa ufunguzi wa Kampeni wa chama hicho,
kisiwani Pemba katika Viwanja vya Tibirizi Chake, Mwenyekiti wa
Ngome hiyo Mkoa wa Kusini Pemba, Halima Ali alisema wanawake
kisiwani Pemba wamejipanga kuhakikisha mgombea wao anashinda kwa
ushindi mkubwa.
“Maalim Seif, sisi tumeshamaliza kazi na kama kampeni isingekuwa sheria sisi tungekwambia usifanye kampeni, lakini kwa kuwa ni sheria fanya tu sisi tumeishamaliza kazi ya kukupa ushindi mkubwa,” alieleza Halima.
Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Chama hicho, Zito Kabwe,
alisema ushindi wa ACT Wazalendo utapendeza zaidi kama wanachama hao wakiwapigia kura wabunge, wawakilishi na madiwani.
Alisema licha ya kuwa yapo majimbo kadhaa wagombea wao wameshaenguliwa na kuwakatia rufaa, lakini watapigana ili warejeshwe kwenye karatasi ya kura.
“Viongozi wenu wa ACT wanaendelea kufanya majadiliano na Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ili kuhakikisha wagombea wetu wa uwakilishi wanarejeshwa,”alisema.
Mapema Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema akipata ridhaa ya kuingia Ikulu Zanzibar, atafanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha biashara.
Alisema CCM ambayo imetawala kwa miaka zaidi ya 50, haijaitendea haki Zanzibar na kuwafanya vijana walio wengi kukosa ajira.
Aliwataka wananchi kutoharibu kura zao kwa kuvipa kura
vyama vingine.
“ACT inasikitishwa sana na umaskini uliopo Zanzibar na nikishaingia madarakani, hilo litakuwa historia hapa
Zanzibar,” alisema Maalim Seif.
Katika hatua nyingine, Maalim Seif alisema Zanzibar itaongozwa kisheria na kila mmoja kupata haki yake, bila ya kujali unyonge wa mtu husika.
“Mwaka 2015, mlikuwa mashuhuda Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,
mliona ilivyopindwa, lakini Serikali ijayo chini ya Maalim Seif
sheria itafuatwa,” alisema.
Aidha maalim Seif alieleza kuwa, hakuna mwananchi yeyote atakayenyimwa haki yake, ikiwemo kitambulisho cha Mzanzibar ukaazi kama ambavyo alidai inafanyika sasa.
Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar alisema, mara akiingia madarakani kwanza atasimamisha kazi ya utoaji wa vitambulisho ya ukaazi vipya kwa kile alichoeleza kuwa watu wengi waliokuwa si raia wa Zanzibar walipewa.
“Hivi sasa wapo watu kutoka nje ya Zanzibar wamekuwa wakipewa
vitambulisho hivyo na kuwakosesha wale wenye haki hiyo,”alisema.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango