Na Israel Mwaisaka,TimesMajira Online, Rukwa
MTANDAO wa Polisi Wanawake TPF-Net Wilayani Nkasi mkoani Rukwa wamewataka wanaume wanaonyanyaswa na wake zao kujitokeza na kupewa msaada wa kisheria ili waweze kupata haki zao.
Wito huo umetolewa kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili ambapo wamesema kuwa licha ya Wanawake na watoto kuwa Wahanga wa vitendo vya ukatili lakini pia bado Wanaume nao wamekua wakinyanyaswa na kukaa kimya.
Katika risala yao wamesema kuwa lengo lao ni kutaka kuona makundi yote yanapewa haki stahili na kuwa Wanawake na Watoto kufuatia misingi iliyowekwa wamekuwa wakinyanyaswa na kuona kwamba hawana mtetezi lakini toka harakati hizi za utetezi zianze angalau wengi wao wanapewa haki zao za kimsingi.
Mmoja wa Polisi hao Miyango Turo amedai kuwa wapo wanawake wakorofi na wanyanyasaji wa wanaume na kuwa umefika wakati sasa kwa wanaume kuanza kujitokeza kuomba msaada pale wanapoonewa badala ya kukaa kimya.
Amesema kuwa Dawati la Jinsia linashughulika na watu wa jinsi zote ili kuweza kuona kuwa kila mmoja anapata haki zake za kimsingi.
Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini Aida Khenan amesema kuwa siku 16 za kupinga ukatili zikawe chachu kwa jamii nzima kuona kuwa mfumo dume unatoweka na kuweka usawa katika jamii na kuweza kuyafikia maendeleo tunayoyataka.
Amesema kuwa yale yaliyofanywa ndani ya siku 16 za kupinga ukatili yakawe ni endelevu na kuona kuwa ni sehemu ya maisha yetu kuendelea kupiga kelele hadi pale tutakapoona vitendo vya kikatili vimetoweka katika jamii
Katibu tawala wa wilaya Cosmas Kuyela kwa upande wake wake amedai kuwa ukatili upo katika Nyanja mbalimbali ambazo zingine hazionekani kiurahisi na kuwa ni jukumu letu kuhakikisha ukatili unatoweka kabisa miongoni mwetu.
Amewataka Wanawake kujikita zaidi katika shughuli za kiuchumi na kuweza kujipatia kipato na kuwa wengi ya Wanawake unyanyasika kutokana na kipato chao kuwa duni na wengi ya Wanaume wameitumia hiyo nafasi ya kiuchumi katika kuwanyanyasa Wanawake.
Siku 16 za kupinga Ukatili zilianza Novemba 25 na kumalizika Desemba 10,2020 zikiwa zimebeba ujumbe usemao “Mabadiliko Yaanza na Mimi”
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea