Na Joyce Kasiki,timesmajira online,Dodoma
MGANGA Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi, amewataka wanataaluma wote wa sekta ya afya nchini kujisajili na kuuwisha leseni kwenye mabaraza yao ya kitaaluma ndani ya miezi sita kuanzia sasa.
Mbali na hilo, amesema kwa wale aliojiendeleza zaidi kitaalam wawasilishe vyeti vyao vya viwango vya taaluma zao kwenye mabaraza hayo ili watambulike kisheria na kitaaluma.
Prof. Makubi ametoa agizo hilo jana jijini hapa wakati akizungumza na wasajili wa mabaraza mbalimbali ya kitaalam ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto pamoja na wasajili wa Bodi zilizo chini ya wizara hiyo.
“Agizo hili ni kwa wanataaluma wote katika sekta ya afya ili muweze kutambulika na uzuri hivi sasa kuna tovuti, hivyo mnaweza kujisajili, kulipia na baadaye kutumiwa vyeti vyenu bila kuchelewa.
Kwa mantiki hiyo nawapa miezi sita muwe mmesajiliwa,”amesisitiza Prof. Makubi.
Amewataka wanataaluma wanaojiendelea kwa ngazi mbalimbali kama vile kwenye shahada za uzamili na uzamivu (PhD) kusajili viwango hivyo katika mabaraza yao ili nao watambulike pia.
“Utaratibu huu umewekwa na Serikali kupitia mabaraza hayo, hivyo kila mwana taaluma anatakiwa kujisajili au kuuwisha leseni ambazo zimeisha muda ili waendelee kutambulika na kufanya kazi zao.” amesema
Aidha, Prof. Makubi amesema Wizara kupitia mabaraza hayo imeweka miundombinu ya mafunzo endelevu ya kitaaluma kwa kila taaluma kwa kufanya mitihani kwa ngazi zote.
Kwa upande wa baadhi ya wadau wa sekta ya afya wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha taaluma bila ya kujisajili kwenye mabaraza ya kitaaluma, Prof. Makubi ametoa miezi mitatu wawe wamejisajili ili watambulike wapo katika kiwango fulani cha taaluma.
“Kuna baadhi ya wataaluma wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha kitaaluma wakati hawajasajili vyeti vyao kwenye mabaraza, nitoe mfano kuna wanataaluma wanaojiita mabingwa wa kitu fulani na wanajitangaza kwa wananchi wakati hatuna ushahidi na kumbukumbu. Kwa hiyo tumekubaliana na mabaraza suala hilo sasa lifikie mwisho na wote waliojiendeleza zaidi waje wajisajili haraka kwa kuwasilisha vyeti vyao.” Alisisitiza Prof. Makubi.
Amewaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa Hsopitali, taasisi za afya, vyuo vya afya na waganga wafawidhi wote kutekeleza maelekezo hayo ili kulinda viwango na hadhi ya taaluma katika sekta ya afya.
“Taaluma zote za afya lazima ziendelee kuheshimika na kusimamiwa vizuri ili kulinda afya za wananchi kwa viwango vya juu na bila kuruhusu wanataaluma bubu,” amesema Prof Makubi.
Katika hatua nyingine pia amewataka waganga wa tiba asili kufuata utaratibu wa kujisajili pamoja na wasaidizi wao na kufuata miongozo ya utoaji wa tiba asili na tiba mbadala.
Amesema Serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano ili kuhakikisha malengo yao ya utoaji wa tiba asili yanafanikiwa.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati