Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga
WAKATI watanzania wakiadhimisha siku ya Homa ya Ini Duniani imeelezwa kwamba wagonjwa wanaougua ugonjwa huo asilimia kubwa hawaoni dalili za moja kwa moja isipokuwa asilimia ndogo.
Hayo yalibainishwa Julai 28,2024 na Daktari kutoka Siha Polyclinic iliyopo jijini Tanga Dkt.Kasanga Bashiru wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku hiyo ambapo wameadhimisha kwa kutoa huduma ya vipimo bure kwa wananchi wa Mkoa huo.
Dkt.Kasanga amesema wenye maambukizi wanapata dalili kali ambazo sio za moja kwa moja zinaweza kufananishwa na magonjwa mengine.
“Kwa dalili ambazo ni viashiria vya moja kwa moja ni homa ya manjano, sehemu za macho na mabadiliko ya ngozi,mikono na kubadilika rangi ya choo pamoja na kukosa hamu ya kula,”amesema.
Amesema kuwa iwapo matibabu ya ugonjwa huo yasipofanyika kwa wakati yanaweza kusababisha ini kufeli na kushindwa kufanya kazi yake ya kawaida hivyo kuleta athari ikiwemo vifo huku akiitaka jamii kuona umuhimu wa kupata chanjo ya ugonjwa huo ili kuweza kukabiliana nao.
“Wakati tunaadhimisha siku ya homa ya ini Duniani ni vema kutoa wito kwa wananchi kuona umuhimu wa kujitokeza kupima na iwapo wakibainika kuwa na ugonjwa huo waanze kuchukua hatua za kukabiliana nao,”amesema.
Akizungumzia umuhimu wa kuchanja chanjo ya ugonjwa huo amesema takwimu zinaonesha kuwa magonwa makubwa ya matatizo ya ini asilimia 45 mpaka 50 yanatokana na homa za ini
“Kuchanja ni kuhakikisha jamii inabaki salama bila kuwa na magonjwa ya homa ya ini (hapatis C,B) kwani hatua za mwanzo hauna dalili zinajitokeza wakati ugonjwa umekuwa mkubwa
Awadhi Abdul kutoka kwenye kituo hicho amesema wameamua kuadhimisha siku hiyo kwa kufanyia watu vipimo vya homa aya ini na kutoa chanjo kama siha wanajitahidi kuhakikisha jamii inapata uelewa katika masuala ya kiafya na kutoa matibabu mbalimbali.
Naye Daktari Jovin Amani amesema dalili za ugonjwa wa homa ya ini ni kujisikia kuchoka na viungo kupata manjano,kupoteza fahamu au kutapika damu hivyo amewashauri watanzania kujitokeza kupima ili kujua afya zao kwa ujumla maana ugonjwa huo unaweza kudambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine .
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja