Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imethibitisha kuwakamata watu wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti zilizochanganywa na bangi iliyosindikwa maarufu kama ‘Skanka’ katika eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa hiyo Jijini Dar es Salaam, leo katika mkutano na Waandishi wa Habari, Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo alisema watu hao walikamatwa baada ya kukutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga ‘Skanka’ na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi.
“Mamlaka katika oparesheni zake imewakamata watu wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti kwa kuchanganywa na Skanka’ katika eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam, kwani katika tukio hilo watuhumiwa hao walikutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga Skanka na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi.
“Hivyo napenda kutoa wito kwa wananchi kuwa makini katika manunuzi ya vitu hususani vinavyopendwa sana na watoto, kama Tomato, biskuti yani cookies, nk. Kwani tumefanya uchunguzi na tumegundua,” amesema Lyimo.
Pia, katika hatua nyingine Mamlaka hiyo, imebainisha kukamata bangi isiyosindikwa kilogramu 423.54, katika oparesheni maalum zilizofanyika hivi karibuni kwenye mipaka na fukwe za bahari ya hindi.
Ambapo Kilogramu 158.54 zikiwa zimekamatwa eneo la Kigamboni na Kawe, zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya mabegi ya nguo tayari kwa ajili ya kusafirishwa.
Huku Kilogramu 265 zikiwa zimekatatwa katika matukio tofauti katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, zikiwa zimefichwa ndani ya magari huku zikichanganywa na bidhaa nyingine ikiwemo maboksi yenye matunda aina ya ‘Apples’ zikisafirishawa kuingia Dar es Salaam.
“Kutokana na jitihada ambazo Mamlaka imeendelea kupambana na masuala ya dawa za kulevya na bangi, tumefanikiwa kukamata Kilogramu 423.54 za bangi iliyosindikwa maarufu kama Skanka’ katika oparesheni maalumu zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za bahari ya hindi,” amesema.
Lyimo amesema, kutokana na oparesheni hizo tayari watu 16 wameshakamatwa ambapo kati yao sita, wameshafikishwa Mahakamani na 10 watafikishwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Aidha, Lyimo ametoa wito kwa wananchi hususani wanafunzi, kuwa makini na vyakula wanavyovutumia na kuacha kuacha kufuata mikumbo isiyofaa ikiwemo kutumia vilevi na vitu wasivyovijua hali ambayo inaweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema, Mamlaka hiyo imebaini kuwepo kwa watu wasiyo waaminifu kwa kuchanganya Skanka’ kwenye vyakula kama Biskuti, Keki, Jamu, Sharubati, Tomato Sauce, pia kwenye Sigara na Shisha.
Ameeleza kuwa, lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha uuzaji wa dawa hizo kwa kificho na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya.
Skanka (Skunk) ni jina la mtaani linaloitambulisha aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu ikilonganishwa na bangi ya kawaida, ambapo dawa hii ya kulevya hutokana na kilimo Cha bangi mseto, ambapo asilimia 75 ni bangi aina ya Sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya Indica.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza