January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaopandisha bei za pembejeo kiholela kukona

Na Isral Mwaisaka, TimesMajira Online, Sumbawanga

SERIKALI Wilayani Kalambo Mkoani Rukwa imewaonya baadhi ya wafanyabiashara wanaouza pembejeo za kilimo kwa bei ya juu tofauti na bei elekezi ya Sh. 61,000 iliyotolewa na Serikali.

Onyo hilo limetolewa na mkuu wa Wilaya hiyo Carlos Misungwi wakati akijibu malalamiko ya baadhi ya wananchi waliokuwa wakilalamikia kupanda kiholela kwa bei ya mbolea kutoka shilingi 61,000 kwa mfuko wa Kilogramu 50 hadi kufikia shilingi 71,000.

Amesema kuwa, wafanyabiashara wanaofanya hivyo washushe bei hiyo mara moja kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria hasa ikiwa bei ya pembejeo hizo zimekwisha wekewa bei elekezi na Bunge la 11, na mpaka sasa Serikali haijatangaza bei mpya hivyo ni lazima itumike bei ileile elekezi na yeyote atakayebainika kuuza kwa bei kubwa basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Amesema, kwakua hivi sasa ni msimu wa kilimo ambapo mahitaji ya mbolea hasa za kupandia na kukuzia yamekuwa juu na ndiyo maana baadhi ya wafanyabiashara wasio waadilifu wametumia mwanya huo kupandisha bei ya mbolea kiholela.

Mmoja wa wakulima wilayani humo, James Simzosha amesema kuwa kutokana na hali hiyo kumeleta usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo huku baadhi yao kulazimika kupanda mazao bila hata kutumia mbolea ya kupandia.

Amesema kuwa, iwapo suala hilo haliotochukuliwa hatua za haraka na Serikali, huenda wakulima wasifanikiwe katika kilimo kwani hakuna muujiza wa kupata mazao mengi na bora bila kufuata taratibu za kilimo bora pamoja na matumizi ya pembejeo za kilimo.

Hata hivyo ameawaomba wakulima wenzake kupaza sauti kwa kutumia njia mbalimbali ili serikali ichukue hatua na hasa ikizingatiwa kua kilimo kinakwenda na muda iwapo muda wa kupanda mazao ukiisha na wakalazimika kupanda bila mbolea watakao umia ni wao wenyewe kwakuwa hawatapata mazao ya kutosha.