December 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaofanya ngono kwenye makaburi kudhibitiwa

Na Elia Ruzika,TimesMajira Online,Dar

ILI kutokomeza vitendo vya uasherati vinavyofanywa na baadhi ya watu katika makaburi ya Sinza (Sinza Makaburuni) wananchi wa eneo hilo wakiongozwa na viongozi wao wamejitolea kufanya usafiri katika makaburi hayo kwa kufyeka vichaka vinavyotumika kufanyia uovu huo.

Hatua hiyo imelenga kushakikisha vitendo viovu vinavyofanyika kwenye makaburi hayo ikiwemo ngono, utumiaji wa dawa za kulevya na uporaji vinatokomezwa.

Usafi katika makaburi hayo umefanywa na wananchi wa maeneo hayo wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Sinza, Raphael Awino pamoja na Mwenyekiti wa Serikali Mtaa wa Sinza A, Ally Mgaya.

Wakazi hao Kata ya Sinza Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam wametumia nafasi hiyo kuuomba uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kutunga sheria kali itakayosimamia ufanyaji wa usafi na utuzwaji wa makaburi yaliyo katika maeneo mbalimbali ili yasitumike kama ngome ya vitendo vya uhalifu kama ambavyo vimekuwa vikifanyika kwenye makaburi hayo ya Sinza.

“Vichaka katika makaburi haya vimekuwa vikigeuzwa maficho ya wanyang’anyi na sehemu rasmi ya kufanyia vitendo vichafu vya usherati au utumiaji wa dawa za kulevya,” amesema mmoja wa wananchi kwa sharti la jina lake kutajwa na kuongeza;

“Hali hii imekuwa ikihatarisha usalama wa wapita njia pamoja na jamii inayoishi jirani na maeneo haya.”

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Shaffi Diwani amesema si jambo la busara kuacha makaburi kwa muda mrefu bila ya kuyafanyia usafi, kwani sehemu hizo wamelala ndugu zetu.

Kwa msingi huo alitoa wito mamlaka za Jiji la Dar es Salaam kutunga sheria ya kudumu itakayowalazimisha wakazi wanaoishi jirani na maeneo ya makaburi kuwa na utamaduni wa kuyahudumia mara kwa mara.

Kwa upande wao Diwani wa Kata ya Sinza, Awino na Mwenyekiti wa Serikali Mtaa wa Sinza, Mgaya walitoa mwito kwa wananchi kujitokeza kuyafanyia usafi makaburi.

Mgaya amesema sio busara makaburi kuachwa bila huduma yoyote na matokeo yake watu wasio kuwa na ustaarabu au wasio na hofu na Mungu wanayafanya kuwa ni sehemu ya kutupa takataka na kufanyia vitendo vingine viovu.

Viongozi hao wamesema zoezi la kuyahudumia makaburi ya Kata nzima ya Sinza litakuwa endelevu sio kusubiri siku maalum au hadi kiongozi atoke Serikali Kuu ili atoe maelekezo ya kusafisha maeneo hayo.

Wametoa wito kwa Serikali kuweka utaratibu maalumu wa kuyawekea ulinzi maeneo ya makaburi ikiwa ni pamoja na kuyajengea uzio ili kulinda hadhi ya wapendwa wetu waliopumzishwa kwenye maeneo hayo.