November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi,Viongozi Musoma vijijini waishukuru serikali ujenzi miradi ya maji

Fresha Kinasa,Times MajiraOnline,Musoma.

WANANCHI na Viongozi wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara wameendelea kuishukuru serikali  ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za miradi  ya maedeleo ikiwemo ya usambazaji wa maji safi na salama katika kata mbalimbali jimboni humo.

Wameyasema hayo hivi karibuni kwa nyakati tofauti mbele ya Mbunge wa Jimbo hilo Prof.Sospter Muhongo ambapo wamesema hatua ya serikali ya kutoa fedha za ujenzi wa  miradi ya maji inamanufaa makubwa katika kuchangia maendeleo yao na kuwaondolea adha kina mama ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Rhoda James Mkazi wa Kata ya Tegeruka amesema kuwa, upatikanaji wa maji ukiwa jirani na makazi ya wananchi  kina mama na watoto wa kike wataendelea kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na hivyo kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.

“Serikali imejitahidi sana kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa kiwango kikubwa jimboni mwetu.  miradi mingi imejengwa  inatoa maji, changamoto ya kuamka usiku  kwa kina mama kutembea mwendo mrefu tukitafuta maji katika  visima imepungua sana,kwa sasa tunatumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo.”amesema Jesca Bwire.

Aisha Mafuru ni  Mkazi wa Kata ya Mugango amesema kuwa, dhamira ya Serikali ya kumtua ndoo mama kichwani kwa kusogeza miradi ya maji jirani na makazi ya Wananchi  imeendelea kuwapa tabasamu wanawake na kuimarisha ndoa zao kwani awali baadhi yakina mama walikuwa  wakiamka alfajiri na kuwaacha waume zao wakiwa wamelala.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof.Sospter Muhongo kupitia taarifa yake aliyoitoa Septemba 28, 2024 amesema kuwa,Wananchi wa kata ya Tegeruka wanatarajia kunufaika na huduma ya maji safi na salama kufuatia mradi wa zaidi ya Shilingi Bil.4 wa kusambaza maji ndani ya Kata hiyo ambao umepangwa ukamilike ndani ya miezi miwili ijayo.

Ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 150,000, unakamilishwa kijijini Mayani kwa ajili ya usambazaji wa maji ndani ya kata hiyo.
Na mabomba ya awali ya kusambaza maji ndani ya Vijiji vyote vitatu vya kata hiyo ambavyo ni  Kataryo, Mayani na Tegeruka yameshatandazwa.

“Kata ya Tegeruka itatumia maji ya bomba kutoka kwenye bomba Kuu la Mugango-Kiabakari-Butiama lililojengwa kwa gharama ya Shilingi Bil.  70.5.   Chanzo cha maji ya bomba hili kiko Kijijini Kwibara, Kata ya Mugango, Musoma   Vijijini.  Mitambo iliyojengwa kwenye chanzo hicho ina uwezo wa kuzalisha maji ya ujazo wa lita Mil. 35, kwa siku.” amesema Prof. Muhongo.

Aidha, maji kutoka kwenye bomba kuu la Mugango-Kiabakari-Butiama  yameanza kutumiwa ndani ya Kata ya Mugango yenye vijiji vitatu. Kijiji cha Nyasaungu cha Kata ya Ifulifu nacho kinatumia maji ya bomba hilo.

Na miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba inajengwa ndani ya Kata za Busambara (vijiji vitatu) na Kiriba (vijiji vitatu) kwa ajili ya kutumia maji kutoka kwenye bomba hilo.Huku Vijiji vyote 68 vya Jimboni mwetu vina miradi ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria. Miradi hii iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.

Prof. Muhongo amesmea kuwa, visima virefu vya maji vinachimbwa kwa baadhi ya vijiji vya Kata ya Bugwema ambavyo miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria itachelewa kuanza kutekelezwa.

Hadi  Septemba 28, 2024,  vijiji 54 kati ya vijiji 68 vya Jimboni mwetu (77.94% ya vijiji vyote) vinatumia maji ya bomba yanayotolewa Ziwa Victoria.