Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Musoma.
WANANCHI wa vijiji vya Mabuimerafuru Kata ya Musanja na Chumwi Kata ya Nyamrandirira Wilaya ya Musoma mkoani Mara wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Hatua hiyo inatokana na juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali za kuwasambazia Wananchi maji hayo ya bomba kutoka Ziwa Victoria.
Ambapo tanki la ujazo wa lita 300,000 limejengwa kijiji cha Mabuimerafuru ambayo yanatumiwa na vijiji vya kata nne ikiwemo Kata ya Musanja Chumwi, Nyamrandirira na Lyasembe Kata ya Murangi pamoja na Masinono Kata ya Bugwema.
Wakizungumzia hatua hiyo Juni 16, 2024 Wananchi hao wamesema, wataondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye visima ambayo yalikuwa si salama kwa matumizi ya binadamu.
“Zamani tulitembea umbali mrefu kutafuta maji visimani, wakati mwingine tulichota maji hayo ambayo pia yalitumiwa na mifugo,”amesema Esta mafuru Mkazi wa Kijiji cha Nyamrandirira.
Aidha Wananchi hao wamesema kuwa, kwa sasa watashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo tofauti na hapo awali ambapo muda mwingi walitumia kutafuta maji.
“Tunafarijika tunapoona miradi ya kijamii itanufaisha moja kwa moja, maji ni uhai yakiwa karibu kina mama wataondokana na kadhia ya kuyafuata umbali na watoto wangu wa kike watahudhuria masomo yao kikamilifu,”amesema Juma Fabian Mkazi wa Mabuimerafuru.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Halfan Haule, amewataka Wananchi hao kutunza miundombinu ya miradi ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu pia kuunganisha maji hayo kwenye kaya zao na kulipia huduma bila kusuasua.
Pia, Dkt. Haule amesema kuwa, miradi hiyo imekuwa ikijengwa kwa fedha nyingi hivyo Wananchi wote wawe sehemu ya kuimarisha ulinzi na usalama kudhibiti hujuma kwa manufaa endelevu.
Vijiji vyote 68 vya Jimbo la Musoma Vijijini vina miradi ya usambaziwaji wa maji ya bomba na iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake