March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WANANCHI WATAKIWA KUTUMIA TAKWIMU KATIKA MIPANGO YAO YA MAENDELEO

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

Wananchi wametakiwa kutumia takwimu rasmi kama nyenzo muhimu katika kupanga mipango yao ya maendeleo, badala ya kuziona kama taarifa za kitaalamu kwa ajili ya serikali pekee.

Wito huo umetolewa na Mtakwimu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Boniface Simpoli, wakati akizungumza katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Simpoli amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina jukumu la kuzalisha takwimu rasmi kwa ajili ya wadau mbalimbali, wakiwemo wananchi wa kawaida, wawekezaji, mashirika ya maendeleo, pamoja na taasisi za serikali na binafsi.

“Takwimu hizi zimegawanyika katika makundi makuu matatu: kijamii, kiuchumi na za kimazingira. Kila kundi lina mchango mkubwa katika kusaidia mtu binafsi au taasisi kupanga mipango ya maendeleo kulingana na mazingira husika,” amesema.

Kwa mujibu wa Simpoli, takwimu za kijamii zinajumuisha Sensa ya Watu na Makazi, makadirio ya idadi ya watu, pamoja na takwimu za afya. Ametolea mfano jinsi ambavyo hata mama lishe anaweza kutumia takwimu hizo kupanga biashara yake.

“Kwa mfano, kwa kutumia takwimu za sensa ya watu na makazi, mama lishe anaweza kujua ni mtaa gani una watu wengi wasiooa au kuolewa, na anaweza kuamua kufungua mgahawa eneo hilo kwa sababu ni dhahiri wengi wao hawapiki nyumbani,” amesema.

Kwa upande wa takwimu za kiuchumi, Simpoli amesema zinajumuisha taarifa kuhusu Pato la Taifa, kilimo, biashara, viwanda na sekta nyingine muhimu. Takwimu hizi hutoa mwelekeo kuhusu maeneo yanayokua kwa kasi, hivyo kusaidia wawekezaji kuamua wapi pa kuwekeza.

“Kwa mfano, sekta ya Habari na Mawasiliano imeonekana kukua kwa kasi zaidi kuliko sekta nyingine kama kilimo, madini au umeme. Maendeleo ya sekta hii yanaweza pia kuchochea ukuaji wa sekta nyingine kwa njia ya mnyororo wa thamani,” alieleza.

Amefafanua kuwa ukuaji wa sekta moja hauimaanishi kuwa sekta nyingine zimedumaa, bali zina kasi tofauti za ukuaji. “Kwa mfano, shule kwenye mtaa zinaweza kubaki tano kwa miaka miwili mfululizo, lakini maduka ya biashara yakiongezeka kutoka matano hadi kumi, hiyo inaonesha kasi ya ukuaji wa biashara,” aliongeza.

Mtakwimu huyo amewahimiza wananchi kutembelea Banda la Takwimu lililopo katika viwanja vya Sabasaba, ili waweze kujifunza zaidi jinsi ya kutumia takwimu kupanga maisha yao na kufanya maamuzi sahihi ya kimaendeleo.

“Takwimu siyo za serikali pekee, ni za wananchi wote. Tujifunze kuzitumia kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla,” alisema.