Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza
Imeelezwa kuwa hali ya unywaji wa maziwa kitaifa kwa mwaka 2023/24,inaonesha kuwa mtu mmoja hunywa lita 67.5 kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo kikilinganishwa na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani(WHO)ambayo yanamtaka mtu mmoja kunywa lita 200 kwa mmoja mwaka.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,ameeleza kuwa sekta ya maziwa nchini inaongezeka kwa kasi ikilinganishwa na miaka ya nyuma,kutokana na ukuaji huo Watanzania waongeze kasi ya kunywa maziwa yaliyosindikwa ili kulinda afya na kufikia kiwango cha cha mapendekezo ya WHO.
“Sasa wapo watu wanakunywa glasi nyingi za bia kuliko maziwa,ushauri unatolewa angalau kwa siku mtu upate glasi moja,nichukue fursa hii kuwahamasisha wananchi wa Mwanza,Kanda ya Ziwa na Watanzania kwa ujumla kuongeza kasi ya unywaji maziwa yaliyosindikwa,yamethibishwa kuwa bora na salama,”ameeleza Mtanda.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ameeleza hayo Mei 29,2024 wakati akifungua maadhimisho ya 27 ya wiki ya maziwa kitaifa yanayofanyika kitaifa mkoani Mwanza uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani hapa yenye kauli mbiu “Kunywa maziwa salama kwa afya bora na uchumi endelevu yalioanza Mei 28 hadi Juni Mosi mwaka huu.
Mtanda amesema sekta ya maziwa katika mwaka 2023/24 kulikuwa na ng’ombe wa maziwa takribani milioni 1.4,ambapo hutoa maziwa wastani wa lita bilioni 3.9 kwa mwaka huku viwanda 130 vya maziwa vikisindika lita milioni 81 za bidhaa hiyo na kuuzwa hapa nchini.
Ambapo mkoani Mwanza sekta ya maziwa inaendelea kukua kwa kasi ambapo ng’ombe wa maziwa waliopo sasa ni 16,223 wastani wa lita 81,115 kila siku kiwango ambacho bado ni kidogo kulinganisha na mahitaji ya wananchi wapatao milioni 3.6.
Kwa mujibu wa Mtanda,mpango uliopo ni kuongeza uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa kupitia Shamba la Serikali la Mwabuki ambalo limepokea majike 500 ya ng’ombe ili wazalishwe na kusambazwa kwa wafugaji wa Kanda ya Ziwa.
“Nitoe wito kwa wafugaji,Watanzania na vijana waliopo Mwanza na Watanzania,kuhamasika na kuingia katika sekta ya ufugaji ng’ombe wa maziwa kwa soko la ng’ombe wa maziwa, soko la maziwa bado ni kubwa.Mkoa una viwanda vidogo 10 vya kusindika maziwa ambapo vinasindika lita 6,000 kwa siku,”ameeleza na kuongeza kuwa;
“Hivi karibuni serikali imewapa fursa vijana wa BBT kufanya uzalishaji wa maziwa na unenepeshaji wa mifugo katika Shamba la Mwabuki,kauli mbiu ya wiki ya maziwa 2024 ‘Kunywa Maziwa salama kwa Afya Bora na Uchumi Endelevu’, nisistize wana Mwanza tuwe na utamaduni wa kupenda bidhaa zilizozalishwa Mwanza kwa kunywa maziwa yaliyozalishwa na viwanda vya ndani ili kutanua wigo wa viwanda vyetu kuimarika na kutengeneza faida na tija,”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TDB,Profesa Zacharia Masanyiwa amesema tasnia ya maziwa inachangia asilimia mbili ya pato la taifa lakini fursa bado zipo nyingi katika sekta ya maziwa na kuwataka wananchi wazichangamkie kwani maziwa ni biashara na lishe pia.
Naye Msajili wa Bodi ya Maziwa,Profesa George Msalya amesema maziwa yanayozalishwa nchini yana thamani ya bilioni 1.3,yana thamani kubwa na mchango mkubwa wa kujenga uchumi wa nchi na ajira ambapo lita 100 zitatoa ajira za kudumu kwa watu wanne.
“Maziwa yanasaidia kujenga uchumi wetu lazima tuyatangaze kwani yana mchango katika uchumi,hapa nchini kaya milioni 2.2 zinajihusisha na uzalishaji na biashara ya maziwa,duniani watu milioni 750 wanazalisha na kufanya biashara ya maziwa,duniani watu bilioni moja wanafanyakazi katika tasnia ya maziwa,”amesema.
Profesa Msalya amesema maadhimisho ya mwaka huu yanatoa elimu ya maziwa na kutambulisha tasnia ya maziwa na ukubwa wake ifahamike kwa jamii,ikachangie katika uchumi,lishe na ajira,hivyo watu waje kupata elimu ya maziwa vinginevyo ukijichanganya maziwa yatawachanganya.
Pia ameeleza kuwa mbali na lita bilioni 3.9 za maziwa zinazozalishwa nchini lakini pia wana agiza mengine kutoka nje wastani wa lita milioni 11.6,na yote yananywewa huku akieleza kuwa wataendelea kuagiza maziwa nje kwa sababu bado hayajatosha.
“Muelekeo wa serikali ni kuhakikisha kwamba tunawekeza zaidi kwenye pingili ya uzalishaji ili tuwe na maziwa mengi nchini na ipo mipango mbalimbali,ikiwemo mradi mkubwa wa kuzalisha maziwa kwa kuangalia mabadiliko ya tabianchi unaokuja na ng’ombe wapya bora 17200 kwa muda wa miaka 10,pia miradi mingine ikiwemo mpango wa uimarishaji programu za chanjo na ulishaji,malisho ili kuongeza uzalishaji;”.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu