Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
MGANGA Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amewataka wananchi kuendelea kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 na kudhibiti magonjwa mengine ya kuambukiza.
Prof. Makubi ametoa wito huo leo alipofanya ziara ya kuona hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Jijini Dodoma.
“Katika kudhibiti ugonjwa wa Covid-19 wananchi walipokea kwa mikono miwili mbinu za kuepuka kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 ikiwemo unawaji mikono kwa maji yanayotirika na sabuni, uvaaji wa barakoa, kuepuka mikusanyiko na misongamano pamoja na mbinu za tiba asilia/tiba mbadala ili kutibu ugonjwa wa Covid-19,” amesema Prof. Makubi
Pamoja na kupungua kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini, Prof. Makubi amesema kuwa bado Watanzania tunatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari za kinga ili hatimae tuweze kutokomeza kabisa ugonjwa wa Covid-19 au pale ambapo bado utaendelea kuwepo tuweze kuishi nao bila madhara makubwa.
Prof Makubi amesema kuwa Serikali inawapongeza wananchi kwa kuipokea na kutumia njia zote zilizotelewa kukabiliana na ugonjwa wa corona pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza na kuwataka wananchi kuendelea na mbinu walizoelimishwa kujikinga na magonjwa ya kuambukiza.
“Mwamko tulio nao sasa hivi wananchi juu ya mbinu hizi tusiziache, tukiendelea nazo zitatusaidia kujikinga na magonjwa mengine” amesisitiza Prof. Makubi.
Hatukuwa na utamaduni wa kunawa mikono mara kwa mara, lakini tuelewe pia usafi wa mikono unatusaidia pia kupunguza hatari ya kupata magonjwa mengine yanayotokana na uchafu yakiwemo magonjwa ya kuhara, au hata kipindupindu.
Prof. Abel Makubi amesema kuwa kufanya mazoezi ya mwili na kula lishe bora yanasaidia pia kujenga afya ya mwili uimara na pia kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na moyo.
“Ni vema wanachi wakaendelea na utamaduni huu huku wakiendelea kupata lishe bora aili kujenga kinga zao dhidi ya mgonjwa mengine” Amesisitiza Prof. Makubi
Kuhusu mbinu ya tibaasili, Prof. Makubi amewapongeza wananchi kwa kuipokea na kuikubali mbinu hiyo katika kusaidia kutibu ugonjwa wa Covid-19 na kutumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzana, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuelekeza bajeti ya tiba asili/mbadala na tafiti za dawa asilia iweze kuongezwa ili kuwawezesha wataalam wanaotengeneza dawa hizo zinazosaidia kutibu magonjwa mbalimbali na kupambana na maambukizi ya virusi vya corona nchini.
Aidha Prof Makubi amewaagiza wataalamu wa afya hasa Wakurugenzi, Waganga wa Mikoa, Wilaya, Maafisa wa afya ngazi za jamii, viongozi wa mashule, vyuo, michezo, na mamlaka za mitaa kuendelea kutoa elimu ya kupambana ugonjwa wa Covid-19 na kuendelea kuhamasisha mbinu za kuudhibiti ambazo zikiendelezwa zitapunguza uwezekano wa kuibuka magonjwa mengine hivyo kuokoa afya za wanachi na fedha nyingi ambazo zingetumika kutibu wagonjwa.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari