January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kuendelea kujihadhari na Corona

Na Martha Fatael,TimesMajira Online. Moshi

HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi, imewataka wananchi wa manispaa hiyo kuendelea kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa wa homa kali ya mapafu Covid-19, kwani jamii imeanza kujisahau na kuendeleza mifumo hatarishi ya maisha.

Manispaa hiyo imetaka tahadhari zinazotolewa na Wizara ya Afya, ziendelee kuwa muongozo sahihi wa kujikinga na ugonjwa huo ambao tayari, Rais Dkt. John Magufuli ameitangazia dunia kwamba ruksa kwa watalii kuingia nchini.

Ofisa Afya wa manispaa hiyo, Sebastian Mgeta alimesema hayo wakati akitoa mafunzo ya siku moja kuhusu magonjwa ya mlipuko, ikiwamo Covid 19 kwa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Kilimanjaro (MECKI) iliyofanyika mjini hapa.

Amesema baadhi ya maeneo yakiwamo ya masoko na mikusanyiko mingine, wananchi wameanza kupuuza tahadhari za msingi ikiwamo kunawa mikopo, kusalimia kwa mikono na kukumbatiana huku baadhi wakionekana kuwa na mafua na kupiga chafya bila kuziba vinywa vyao.

“Pamoja na taarifa zilizotolewa na serikali, lakini ni muhimu kwa jamii kujikinga na ugonjwa huu ni vizuri kutoa taarifa iwapo kuna watu wana dalili za mafua na magonjwa mengine ya mlipuko, ili serikali ichukue hatua mapema kabla ya athari kuongezeka,” amesema.

Amewataka waandishi wa habari, kuandika habari kwa kuzingatia sheria zinazosimamia utoaji wa taarifa za magonjwa ya milipuko duniani, kwani kinyume na hapo wanaweza kuliingiza taifa katika taharuki kubwa.