Na Mwandishi Watu,Timesmajiraonline, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama, amewataka wananchi kuchukua Tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Octoba hadi Disemba mwaka 2023, baada ya Mamlaka ya hali hewa nchini (TMA) kutoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli zinazotegemewa kuanza katika kipindi hicho, ambao umeonesha uwepo wa El-Nino itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo 31 Agosti 2023, alipokuwa akizungumza na waandishi habari katika Ukumbi wa Mkutano wa Ofisi ya hiyo mtaa wa Posta Jijini Dodoma.
Waziri Mhagama amesema kipindi hicho cha mvua kubwa kinaweza kuendelea mpaka mwezi Januari 2024, na amesema kuwa Msimu wa Vuli ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka unahusisha maeneo ya Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kusini mwa mkoa wa Simiyu, Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.
“Tunaona madhara kadhaa yanayoweza kutokea katika baaadhi ya sekta kutokana na uwepo huo wa El-nino utakaosababishwa na mvua kubwa katika kipindi hicho ambacho kimesemwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini ni kama vile, mafuriko yatakayoleta uharibifu wa miundombinu, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali na maporomoko ya ardhi kuathiri makazi,”amefafanua Waziri Mhagama
Aidha, ameongeza kusema kuwa madhara mengine yanaweza kutokea katika Sekta ya mazingira ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mashamba, Miundombinu ya usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini pamoja na magonjwa ya milipuko kwa binadamu, wanyama na kuongezeka kwa wadudu waharibifu wa mazao na mimea.
Sambamba na hilo, Waziri Mhagama amesema Serikali inaelekeza kamati za usimamizi wa maafa na sekta, kushirikiana na umma kuchukua baadhi ya hatua kama vile kutambua maeneo hatarishi na yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuandaa mipango ya kuzuia madhara na kukabiliana na maafa endapo yatatokea pamoja na kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.
“Tunazielekeza kamati hizo zisisubiri maafa yatokee, waanze kutambua maeneo yote hatarishi na yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuanza kuandaa mipango ya kuzuia madhara yoyote yanayoweza kutoka na utabiri huo wa Mamlaka ya hali ye hewa,”amesitiza Waziri Mhagama
Pia ameziagiza kamati hizo kuanza kuandaa na kuainisha rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikiksha zianaendana na maeneo yao.
Awali Waziri Mhagama amezikumbusha kamati hizo kuchukua hatua kwa kuzingatia utabiri wa Hali ya Hewa kwa kuelimisha wananchi kwenye maeneo yao juu ya hatua za tahadhari za kuchukua ili kuokoa maisha pale ambapo jambo lolote litatokea na kukoa mali na kutoa taarifa kwa haraka sana kwa mamlaka Husika kuhusu dalili zozote za kutokea Maafa.
Waziri Mhagama Ametoa wito kwa wananchi wote wanaoishi na kuendesha shughuli za kiuchumi maeneo ya uwanda wa chini na pembezoni mwa mabonde ya maji wanatahadharishwa kuchukua hatua ili kunusuru maisha na mali zao.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba