November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kuacha kujenga maeneo ambayo hayajapimwa

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula amewataka wananchi kuacha kujenga katika maeneo ambayo hayajapimwa.

Huku akitoa wito kwa wazee kuwa mabalozi kwa wenzao kwa kuwaelimisha kuacha kujenga bila ya kuwa na kibali.

Dkt.Angeline ameyazungumza hayo wakati alipo kutana na wazee wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikiwa ni kundi la pili ambao wamepata mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022, na mapambano dhidi ya ukatili yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani hapa.

Ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kuacha tabia ya kufanya ujenzi katika maeneo ambayo hayajapimwa kwani miji haipangiki imekaa vibaya barabara hazijulikani zinapita wapi na ukitaka kupitisha bomba ni ugomvi,barabara ni ugomvi mtu ataki kutoa eneo lakini ikitokea ajali ya moto namna ya kuzima moto ni shida japo hawaombei.

Hiyo ameeleza kuwa ni lazima sasa wasonge mbele kama Wizara wameisha toa muongozo katika maeneo yote ambayo yanakua kwa kasi wanawawezesha viongozi wake kuwa na miongozo itakayowaelekeza waweze kuwapanga watu wao,

“Wote ni wazee hapa mliona vijiji vya ujamaa vya miaka 74 hatukua na sheria ya mipango miji,lakini ukienda kwenye vile vijiji vilipangika,nyumba moja kwenda nyingine kulikuwa na nafasi,maeneo ya barabara yalikuwepo,maeneo ya soko yalikuwepo, shule watenga lakini ile sheria haikuwepo, kwanini Mwalimu Nyerere aliweza kufanya hivyo kwanini sisi tusiweze,”ameeleza Dkt.Angeline.

Aidha ameeleza kuwa kwa Ilemela hapa hakuna mtu anayeweza kujenga bila kupata kibali cha ujenzi kwani ni Halmashauri na haina vijiji.

“Manispaa haina Kijiji watu wanajijengea tu mkiwekewa ‘X’ ya kubomolewa mnaanza kupiga kelele kwa Mbunge,naomba kupitia nyie wazee tuache kujenga, tuwaambie na majirani zetu huko mlipo asijenge bila kibali hii ni Manispaa ipo chini ya mipango miji na hapo tutajikuta tumekaa vizuri,”ameeleza Dkt.Angeline.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Mohamed Yusuph, ameeleza kuwa jambo la kutojenga katika maeneo ambayo hayajapimwa ni zuri.

Kwa sababu kwa sasa kumekuwa na ugomvi kuhusu kuachiana nafasi katika upimaji shirikishi kati ya jirani na jirani hali inayochangia kukosekana na barabara na endapo ikitokea majanga ya moto mtu anashindwa kupita kwa ajili ya kufanya uokoaji.

“Kiukweli ujenzi holela kwa Manispaa yetu haikubaliki katika mipango miji kipindi cha ujamaa sheria haikuwepo ya mipango miji lakini watu walijipanga vizuri na miundombinu ilikuwa vizuri je sasa hivi kuna teknolojia na vijana wamesoma basi tusisubilie serikali itupange nashauri wale ambao wanawauzia watu maeneo husika basi wawe wanajali sehemu zile za barabara waweke wazi hata kabla ya serikali haijafika, na serikali ije tu kutuelekeza namna tutakavyokuwa tunakaa na kujipanga,”ameeleza Yusuph.

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula akizungumza wakati alipo kutana na wazee wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikiwa ni kundi la pili ambao wamepata mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022, na mapambano dhidi ya ukatili yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani hapa.(Picha na Judith Ferdinand)
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mohamed Yusuph, akizungumza wakati Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula alipo kutana na wazee wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikiwa ni kundi la pili ambao wamepata mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022, na mapambano dhidi ya ukatili yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani hapa.(Picha na Judith Ferdinand)