December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi waombwa kumuunga Mkono Rais Samia

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam.

CHAMA cha Mapinduzi CCM, kimewaomba wananchi kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita na kudai kuwa hadi sasa imeonekana kufanya vizuri, katika kuhakikisha inatekeleza yale yote iliyoahidi katika ilani ya chama hicho.

Rai hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Daniel chongolo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kawe, katika Viwanja wa Tanganyika Pekazi ukihusisha mikoa mitatu Dar es Salaam, Morogoro na Pwani.

Chongolo amesema, CCM inaridhishwa na namna Serikali inavyofanya kazi yake vizuri, ikidai kuwa yale yote yaliyoahinishwa katika Ilani ya chama yameshatekelezwa kwa asilimia kubwa ikiwa pamoja na uboreshwaji katika upande wa elimu, afya, miundombinu ya barabara, umeme ikiwa pamoja na kuwaangalia wafanyabiashara wadogo (machinga).

“Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huu ni wazi kuwa wote hapa tunamuunga mkono Rais wetu Mh Samia Suluhu Hassan..basi wakati nakuja hapa niliwasiliana na Rais na akasema niwape salamu kuwa anawapenda sana na kasema atafuatilia mkutano mwanzo mwisho.

Pia ameniomba niwaambie kuwa Chama cha CCM bado kinaendelea kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa katika irani ya chama moja baada ya lingine ili kuhakikisha inatatua changamoto na kuboresha maisha ya wananchi katika mikoa yote mitatu ikiwa Mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro na Pwani kama inavyofanya kwa nchi nzima”, amesema Chongolo.

Pia katika mkutano huo, uliohudhuriwa na wananchi wengi, Chongolo alizungumzia suala la bandari DP Word na kudai kuwa, jambo linaloendelea hivi sasa baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai ni jema na kuwaomba wananchi wasiwasikilize wapotoshaji wanaodai kuwa bandari inauzwa.

Aidha kwa upande wa maeneo ya maegesho ya magari katika maeneo yote nchini, CCM imeahidi kuliangalia upya suala hilo na kudai kuwa itahakikisha inatenga maeneo sahihi na ya kutosha ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.

“Suala la parking! Hili nalo limekuwa tatizo sana, mtu kapaki gari yake alafu anakuja mwingine anamkamata kuwa ni wrong parking haya hiyo sehemu ya parking sahihi umemuwekea wapi?! Inabidi maeneo yaweke ya kutosha kwa ajili ya parking na sisi kama chama cha siasa hatuwezi kuacha watu wanaonewa hivyo Hilo nalo litafanyiwa kazi ndugu wananchi niwaondoe hofu” ameongeza Chongolo.