Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline, Ruvuma
WAKAZI wa Kijiji cha Lutukila Halmashauri ya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kupima upya mpaka wa Shamba la Mwekezaji ili kutoruhusu mgogoro kati yao na Kampuni ya Jenga Tanzania anayemiliki ekari 50,000.
Wamesema kuwa mpaka huo unamega ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 3000 ambazo wakazi wa kijiji hicho wanaitumia kwa shughuli zao.
Akizungumza na waandishi wa Habari Mwenyekiti Mstaafu wa kijiji hicho, Christian Mapunda amesema kabla ya mwekezaji wa sasa kuuziwa shamba hilo, wananchi walitoa arhi hiyo kwa mwekezaji wa kwanza ambaye aliahidi kuwafanyia mambo kadhaa ya kimaendeleo.
Amesem Mwekezaji huyo aliwaleta maofisa ardhi kutoka wilayani ambao walipima shamba hilo na kuweka mpaka ambao ulikataliwa na wananchi na hivyo wakatakiwa kuufanyia marekebisho.
Amesema Maafisa ardhi walipofika kufanya marekebisho ya mpaka walihamisha mawe ya mpaka na kuyapeleka mahali ambapo wananchi walitaka yawekwe, lakini wataalam hao hawakubadilisha majira nukta (GPS).
Amesema baada ya miaka mingi kupita, mwekezaji wa kwanza amemuuzia mwekezaji mwingine ambaye sasa amefika kuhakiki mpaka wa shamba lake kwa kutumia Majira ya nukta ambayo yanaonyesha mpaka wa awali ambao awali ulikatawa na wananchi.
“Chanzo cha mgogoro huu ni Maofisa Ardhi wa Halmashauri ambao wakati wakifanya marekebisho ya mpaka walihamisha mawe kwa lengo la kuwaridhisha wananchi lakini hawakubadilisha kurekebisha GPS jambo ambalo kwa sasa linaanzisha mgogoro baina ya wananchi na mwekezaji mpya” amesema Mapunda.
Kwa upande wake Cornel Mbilinyi ambaye ni mkazi wa kijiji hicho cha Lutukira amesema jitihada za wananchi kumfahamisha mwekezaji mpya na kumtaka aheshimu makubaliano na mpaka wa awali lakini mwekezaji amegoma na badala yake anataka kuchukua ardhi yao kuwa sehemu ya shamba lake.
“Mwekezaji anasema hati anayoilipia Serikalini inamtaka alipie eneo lote ikiwemo mashamba yetu, hivyo hawezi kutuachia ardhi yetu ndio sababu tunaiomba Serikali itusaidie kutatua suala hili” amesema Mbilinyi.
Mkazi mwingine wa kijiji cha Lutukira, Steven Nyoni amesema wao kama wananchi hawapingi uwepo wa Mwekezaji na akadai kuwa wanampenda awepo kwenye kijiji hicho kwa vile anashiriki katika shughuli za maendeleo, lakini wanataka aheshimu mpaka wake kwa kuhakikishi haingii kwenye ardhi ya wananchi.
Hata hivyo hivyo amesema Serikali inapaswa kuingilia kati suala hilo kwa kufika kijijini hapo kurekebisha mpaka wa shamba la mwekezaji ili waishi naye kwa amani na utulivu.
Akizungumzia suala hilo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Songea , Katibu Tawala Wilaya ya Songea, Mtela Mwampamba amekiri kuutambua mgogoro huo na kudai kuwa madai ya wananchi ni ya msingi.
Amesema baada ya kupokea malalamiko ya wananchi Serikali imeanza utekelezaji kwa kuwaagiza maofisa Ardhi wa Halmashauri ya Madaba kwenda kurekebisha mpaka wa shamba hilo ili kuepusha mgogoro baina ya wananchi na mwekezaji huyo.
“Tumepokea malalamiko ya wananchi na kwa hakika madai ya wananchi ni ya msingi, Serikali haijashindwa kushugulikia mgogoro huo na tayari ofisi ya Mkuu wa Wilaya imeshaanza utekelezaji kwa kuwaagiza maofisa Ardhi wa Halmashauri ya Mdaba kwenda kurekebisha mpaka wa shamba hilo kwa kuzingatia matakwa ya wananchi,” amesema Mwampamba.
Wakazi wa kijiji cha Lutukira walitoa ardhi yao yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50,000 kwa mwekezaji tangu mwaka 1991 kwa sharti la kumtaka mwekezaji huyo wanunulie trekta la kilimo na kuwafanyia mambo mbalimbali ya kimaendeleo, lakini hawajawahi kutekelezewa ahadi hizo na badala yake wananchi hao wako hatarini kuporwa ardhi yao nyingine yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 3200.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi