September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wametakiwa kupunguza ulaji wa vyakula vya sukari

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Wananchi mkoani Mwanza,wametakiwa kupunguza ulaji wa vyakula vya wanga na sukari, ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa maumivu ya viungo vya mwili.

Kwa mujibu wa Mtaalamu wa Mazoezi Tiba,wa kituo cha afya Salaaman, Dkt.Emmanuel Nyagabona, ameeleza kuwa,kwa sasa kumekuwa na changamoto ya maumivu ya viungo kwa binadamu bila kujali umri.

Dkt.Nyagabona,amezungumza hayo Septemba 6,2024, wakati wa uzinduzi wa kambi ya matibabu ya bure inavyofanyika kwa siku mbili Septemba 6 na 7,mwaka huu,ilioandaliwa na kituo hicho cha afya Salaaman kilichopo Kata ya Mirongo jijini Mwanza,ambapo ameeleza changamoto hiyo ya maumivu ya viungo shida ni kutokana na kula kwa wingi vyakula vyenye sukari

“Lishe yetu imekuwa na matumizi makubwa ya sukari na chumvi,na ili mwili kumengenya sukari,kwa ajili ya kupata nguvu ,tunatakiwa kuwa na madini ya ‘calcium’,.Kwa sababu vyakula vingi tunavyokula vinakuwa havina calcium,kwaio mwili unaenda kuchukua calcium maeneo mengine ikiwa ni pamoja na mifupa,figo na ini,”ameeleza Dkt Nyagabona na kuongeza:

“Sasa ikichukuliwa ‘calcium’ kwenye mifupa, inapata upungufu wa madini hayo,inakuwa rahisi mifupa yako kusagika,kuvunjika na kupata changamoto ya mifupa na inachangia maumivu ya viungo.Hii ni kutokana na utaratibu wa vyakula tunavyokula tumekuwa tukitumia wanga na sukari kwa wingi zaidi,utakuta kwenye jamii za kiafrika ugali ni mkubwa huku mboga ikiwa ndogo.Ni vizuri watu wakashauriwa juu ya lishe kwa kuhakikisha katika milo yao sehemu kubwa wapate protini,matunda ,mbogamboga na wanga kidogo,”.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa lengo la kituo hicho cha afya Salaaman,kufanya kambi hiyo ya matibabu ni kutokana na uwepo wa ongezeko la magonjwa mbalimbali ikiwemo maumivu ya viungo,macho,shinikizo la damu na mengine.Ambapo ameeleza kuwa makadirio ya chini kwa siku hizo mbili wanatarajiwa kufikia wananchi takribani 600.

Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Afya Salaaman,Daktari Abushiri Katunzi, ameeleza kuwa kituo hicho kina miaka 16 tangu kuanzishwa kwake, huku huduma kama hizo walikuwa wakitolea ndani.Ambapo wajawazito wanapata huduma za kliniki bure, pamoja na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao wanahitaji msaada wamekuwa wakiwapati huduma bure bila malipo.
Lakini kwa mwaka huu baada ya kuona wametoa huduma hizo kwa muda mrefu wameona waitoe nje ili kuweza kufikia wengi.

Akizindua kambi hiyo ya matibabu katika kituo cha afya Salaaman,Diwani wa Kata ya Mirongo,Hamidu Said, ameeleza kuwa kituo hicho cha afya,kimeunga mkono juhudi za serikali katika utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Said ameeleza kuwa katika Kata yake ya Mirongo,kuna vituo vya afya zaidi ya vinne,hivyo amewahimiza wengine waige mfano wa Salaaman licha ya kuwa kituo cha afya Makongoro kimekuwa kikifanya jambo kama hilo kwa muda mrefu.

“Wananchi wajitoke kwa wingi,kwani kugundua afya yako ni jambo la msingi,kila mmoja nauhitaji katika suala la afya.Pia kituo chetu cha Makongoro kimekuwa kikifanya vizuri na huduma ni nzuri kwa gharama nafuu.Ambapo mpaka sasa hivi kituo chetu cha Makongoro kina zaidi ya milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wake,fedha kutoka serikali Kuu,”.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata matibabu katika kituo hicho cha afya cha Salaaman,akiwemo Dorice Kasusu,ameeleza kuwa,kipato dunia, gharama za matibabu ndio chanzo cha wananchi kutokuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara.Pia afya ikiwa dhaifu,huwezi kufanya jambo lolote hivyo huchangia umaskini katika familia.

Damas Silayo, ameeleza kuwa sababu ya wananchi wengi kutojitokeza kupima afya zao ni kutokana na gharama za vipimo na matibabu kuwa juu ukilinganisha na vipato vyao halisi.

“Tunafurahi kwa fursa hii,iliotolewa na kituo hiki cha afya ya kutoa huduma ya kupima afya na matibabu bure,kwani itatusaidia kujua afya zetu,”.