March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wametakiwa kujitathimini kabla ya kuchukua Mikopo

Na Bakari Lulela,Timesmajira

Mkurugenzi mtendaji wa SELF Microfinance Bi. Santieli Yona amewataka wananchi kabla ya kukopa wafanye tathmini ya kina kuhusu matumizi ya fedha wanazozichukua kwa ajili ya shughuli zao kwani wakijipanga vema watakuwa na uhuru,kujiamini pamoja na kuweza kurejesha mikopo yao bila matatizo  yeyote.

Akizungumza kwenye kikao na jukwaa la Wahariri na Waandishi wa Habari Morroco jijini Dar es salaam Santieli amebainisha kuwa kuna changamoto ya wananchi wengi kukosa elimu ya fedha na kushindwa kufanya tathmini kabla ya kukopa ambapo husababisha baadhi wa watu wawe na hulka ya kutojali urejeshaji wa mikopo waliyoichukua.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa suluhuhisho la kuzishinda changamoto za fikra potofu za ukopaji ni muhimu kuweka mkazo katika utoaji elimu kwa raia ili kuimarisha huduma za fedha kwa kuwa elimu hiyo imewafikia wachache.
Aidha bi Santieli alifafanua mafanikio  ya SELF ikiwa ni kutoa mikopo kwa ajili ya nishati safi ya kupikia ili kutekeleza agenda ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na manufaa ya mikopo hiyo  itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi.

  “Moja ya mafanikio tuliyoyapata ni kutengeneza ajira,sisi tunatoa mikopo kwa taasisi zinazokopesha na wajasiriamali sasa wanapopewa fedha, wanajiajiri na kutoa fursa kwa watu wengine na katika kipindi hiki tumeweza kutoa ajira zipatazo 183,000, jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa Taifa, kwani si serikali pekee inayoweza kutoa ajira, bali kila mmoja anaweza kujiajiri na kujikimu.,”ameeleza

Hata hivyo ameongeza kuwa Microfinance yao inatoa elimu ya fedha mara kwa mara kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo maonesho ya Nanenane, Sabasaba, makongamano na kupitia vyombo vya habari lengo  ni kuhakikisha wananchi wengi wanafikiwa na kusaidiwa kifikra kuhusu mikopo.

“Tuna dhamira ya kufika kila mkoa na tunawaalika Watanzania waje kushiriki na sisi kwa sababu hatuwezi kwenda peke yetu ila na wao pia huwa tunafuatilia na kuona kama huduma zetu zinabadilisha maisha ya wanufaika na niwajuze kila baada ya muda tunapenda kujua walikuwa wapi  na mikopo imenufaishaje na wapo viwango gani sasa ,” amesema Santieli 

Taasis hiyo ya kifedha imelenga kuongeza mtaji wa mikopo hadi Tsh 300 billion ndani ya miaka mitano ijayo na itawafikia zaidi ya wanufaika 20,000 moja kwa moja ambapo imeweza kujenga uwezo kwa taasisi 549 kwa kutoa ushauri mbalimbali.