Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
WITO umetolewa kwa Wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya Alama za Taifa ikiwemo Ngao ama Nembo ya Taifa, Bendera ya Taifa na Wimbo wa Taifa na kuendelea kujifunza matumizi sahihi ya alama hizo pamoja na matumizi ya Gazeti la Serikali
Hayo yamesemwa mapema Machi 20,2025 na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali George Lugome kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, alipokuwa akizungumza na chombo kimoja cha Habari Jijini Dar es Salaam.
Lugome amesema kuwa hivi karibuni kumekuwa na upotoshwaji wa Alama za Taifa na kukumbusha kuwa Alama hizi zipo kwa mujibu wa sheria “Na yeyote atakayechezea alama hizi atapata adhabu kwa mujibu wa sheria na adhabu yake kwa yeyote anayekiuka atatumikia kifungo cha miaka miwili Jela ama faini,ama vyote viwili kwa pamoja, ambapo sheria hii ya mwaka 1964 ipo kwenye mchakato wa kubadilishwa,”amesisitiza.
Akizungumza kuhusu Nembo ya Taifa, Lugome amesema kuwa Nembo hiyo, ipo kwa Matumizi ya shughuli za Serikali pekee na sheria imesema Wazi, na aliongeza kwa kusema kuwa matumizi ya alama za Taifa ambayo siyo sahihi yanaharibu Haiba ya Taifa na Idara ya Mpiga Chapa ndo yenye jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa matumizi ya Alama hizi yanatumika kwa usahihi.
Aidha, Bwana Lugome amefafanua kuwa uchapishaji holela wa alama hizi na uchoraji wa nembo hizi kuonesha ubunifu wao, unachangia upotoshwaji na kuharibu uhalisia wake.
Kwa Upande wa Bendera ya Taifa,Lugome Alizungumza na kutolea ufafanuzi kuhusu rangi nne za Bendera ya Taifa zinazotumika
Akizungumzia Wimbo wa Taifa,Lugome amesema Wimbo wa Taifa Unavyoimbwa lazima uimbwe kwa beti zote mbili na kufuata Ala zilizowekwa na kusimama kikakamavu ambapo ni hali ya kuonesha utamaduni na Uzalendo kwa Taifa hili.
Kwa upande wa Gazeti la Serikali amesema kuwa, ni jarida Linaloratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na Kuhaririwa na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, ambapo linachapishwa mara moja kwa wiki na kujikita katika kutoa taarifa Muhimu za Serikali hususan Utendaji wa Serikali na Taarifa Binafsi, na Jarida hili lipo kwa Mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, na kanuni za kudumu za Utumishi wa umma kanuni C27-30.



More Stories
Kamati ya kudumu ya Bunge yapongeza ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati Mtumba
Gawio kutoka kampuni ambazo Serikali ina hisa chache zapaa kwa asilimia 236
Pinda:Vijana tumieni fursa kupata maarifa ya ufundi stadi