Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
JAMII imeombwa kutembelea Banda la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo katika Maonesho ya 48 ya kimataifa ya Biashara sabasaba ili waweze kufanya uchunguzi na kujua afya yao.
Wito huo umetolewa na Daktari wa Moyo kutoka (JKCI) Marsia Tillya, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho hayo.
“Ni vizuri mtu kujua afya yako kabla tatizo halijatokea hivyo, tunawakaribisha waje kwenye banda letu tunatoa elimu na watakutana na madaktari tofauti,” amesema Dk. Tillya.
Akizungumzia kuhusu maonesho hayo Dkt Tillya amesema katika Maonesho hayo wananchi wananchi
883 kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa jirani wamefanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo.
Amesema kati yao 196 wamefanyiwa kipimo kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO), 212 kipimo cha umeme wa moyo (ECG) na wengine wamepimwa uzito, kisukari na kupewa ushauri kuhusu lishe.
“Kupitia maonesho haya watu 61 wamepewa rufaa kwa uchunguzi zaidi ya baadhi ya watu walioonwa wamebainika kuwa magonjwa ya milango ya moyo ambao wamepewa rufaa kwenda katika taasisi hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi na matibabu endelevu”amesema
Amesema wengine wamebainika kuwa na presha lakini hawajui, wenye uzito uliopitiliza na wenye kisukari.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano JKCI, Anna Nkinda, amesema watu hao wamehudumiwa tangu yalipoanza maonesho hayo na wanatarajia idadi itaongezeka kutokana na kuwapo kwa mwitikio mkubwa.
Amesema wanashiriki katika maonesho hayo kwa kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo ambapo wanapima vipimo vya damu, kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo, vipimo vya sukari, uzito na ushauri wa lishe.
“Tunaomba wananchi waje Sabasaba katika banda letu kwa sababu huduma tunazotoa tumepunguza gharama, watapata ushauri wa jinsi ya kutumia dawa za moyo, ushauri wa lishe na tunao madaktari wa watu wazima na watoto,” amesema Nkinda.
Aidha amesema katika maonesho hayo wanawaelekeza watu namna ya kupata huduma ya tiba mtandao ambapo mgonjwa anaweza kutibiwa kokote aliko kwa kuchagua daktari anayemtaka.
Nkinda amesema pia wana huduma ya matibabu ya moyo kwa wagonjwa majumbani ambapo mgonjwa hupewa kifaa maalumu kinachowekwa chini ya kitanda chake ili kufuatilia presha, oksijeni na umeme wa moyo ambacho kimeunganishwa na simu ya daktari anayemtibu.
“Kama kukitokea tofauti yoyote kifaa hutuma taarifa kwenye simu ya daktari kisha atawapigia simu wanaomuuguza wampe huduma ya kwanza wakati huo tunatuma gari la wagonjwa liende kumfuata na kumleta hospitali,” amesema Nkinda.
Mmoja wa wananchi waliopatiwa huduma katika banda la JKCI, Juma Mpanda, amesema; “Nilikuja Dar es Salaam kwa shughuli za kibiashara lakini nilisikia matangazo kwamba kutakuwa na huduma ya kiafya hivyo, niliona nipite kwanza kwenye afya halafu niendelee na mambo mengine…nimepokelewa vizuri, nimefanyiwa vipimo vizuri kwa kweli wako vizuri na bei zao ni nafuu.
More Stories
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa