December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi waanza ujenzi wa zahanati yao

Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Mara.

WANANCHI wa Kijiji cha Kaburabura Kata ya Bugoji Wilaya ya Musoma mkoani Mara wameamua kuanza ujenzi wa zahanati ya kijiji chao ili waweze kupata huduma za afya kijijini hapo.

Umbali mrefu wa kutembea kwenda kupata huduma za afya katika Kijiji Cha Bugoji unatajwa ni moja ya sababu kuu iliyosababisha wananchi wa kijiji hicho waamue kujenga zahanati yao.

Ambapo Kijiji cha Kaburabura ni moja ya vijiji vitatu vya kata ya Bugoji ambavyo vyote vinatumia zahanati ya Kijiji Cha Bugoji.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijiji Mei 23, 2024,ambapo imesema kuwa tayari Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijiji Prof. Sospeter Muhongo ameshafanya harambee ya kupata fedha na vifaa vya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho ili kuwaunga mkono wananchi hao.

Huku pia wananchi jimboni humo wakitajwa kuendelea kuchangia nguvu kazi, fedha taslimu na vifaa vya ujenzi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo
Ikiwemo inayobuniwa na kuanza kutekelezwa na wao wenyewe ya ujenzi wa zahanati na shule mpya kwa faida yao.

Jimbo la Musoma Vijijini lina jumla ya Kata 21 zenye Vijiji 68 na Vitongoji 374,ambapo zahanati 29 zinatoa huduma za afya kati ya hizo 25 ni za Serikali na 4 ni za binafsi huku Vituo vya Afya vikiwa sita pamoja na
Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ikiwa ni moja.

Taarifa hiyo imesema, Zahanati mpya 16 zinajengwa jimboni humo na Wananchi kwa kutumia michango ya fedha na vifaa vya ujenzi kutoka kwenye kaya za Vijijini mwao, Mbunge wa Jimbo, Madiwani na Viongozi wengine wa Vijiji na kata zenye miradi ya ujenzi.

Wengine ni baadhi ya Wazawa wa Vijiji na Kata zenye miradi ya ujenzi na Serikali Kuu hutoa michango ya kusaidia ukamilishaji wa zahanati zinazojengwa na Wananchi katika vijiji vyao.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijiji Prof. Sospeter Muhongo, amewaomba wadau wa maendeleo jimboni humo kuunga mkono juhudi za wananchi na Serikali kwa kusaidia ujenzi wa zahanati ili wananchi wasitembee umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Neema Mafuru Mkazi wa Kata ya Bugoji amesema kuwa, huduma za afya zinapokuwa karibu na wananchi ni hatua muhimu ya kuokoa maisha yao hasa wajawazito.

“Tumekuwa tukishirikiana na Mbunge wetu Prof. Muhongo katika miradi ya maendeleo hasa miradi ya elimu na afya lengo ni kujileta maendeleo pia serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya jimboni kwetu na sisi Wananchi kwa upande wetu tunawajibika,”amesema Julius Maira Mkazi wa Bugoji.