

Na Joyce Kasiki, Tanga
Wananchi wa mkoa wa Tanga wameaswa kujitokeza kwa wingi kushiriki Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika viwanja vya Usagara ili kunufaika na elimu ya fedha pamoja na fursa mbalimbali za mikopo zitakazowasaidia kujiendeleza kiuchumi.
Wito huo umetolewa Januari 20, 2026, na Meneja Masoko na Uhamasishaji wa Mfuko wa SELF, Linda Mshana, wakati akizungumza na wananchi waliotembelea banda la mfuko huo katika maadhimisho hayo yaliyoanza Januari 19 na yanatarajiwa kumalizika Januari 26, 2026.
Mshana amesema maadhimisho hayo yamelenga kuwajengea wananchi uelewa sahihi kuhusu matumizi bora ya mikopo, mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kukopa pamoja na maswali ya msingi wanayopaswa kuuliza wanapohusiana na taasisi za kifedha, ili kuepuka mikopo yenye riba kubwa isiyokuwa rafiki kwao.
Ameeleza kuwa Mfuko wa SELF unaendelea kutoa mikopo ya aina mbalimbali ikiwemo mikopo kwa wafanyabiashara wa sekta ya nafaka, wakulima, wafugaji na wavuvi, sambamba na mikopo ya kuboresha makazi kwa wananchi wanaotaka kuboresha nyumba zao.
“Pia tunatoa mikopo kwa taasisi za kifedha ambazo tayari zimeanzishwa na zina kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa lengo la kuongeza mtaji na kuziwezesha kuhudumia wananchi wengi zaidi,” amesema Mshana.
Ameongeza kuwa maswali kuhusu riba yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kwa wananchi wengi, hali inayoonesha bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu ya fedha, hususan katika kukokotoa riba na kuelewa masharti ya mikopo.
Mshana amesisitiza kuwa SELF itaendelea kutoa elimu na mafunzo ya masuala ya kifedha na bima kama sehemu ya jitihada za Serikali katika kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.
Amefafanua kuwa Mfuko wa SELF ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha, inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo yenye masharti nafuu na elimu ya fedha kwa maendeleo endelevu.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama