Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Mbambabay
WANANCHI wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wamemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 12.2 kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya ya Ndumbi ziwa Nyasa.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya akizungumza mjini Mbambabay amesema ujenzi wa bandari hiyo umekamilika kwa asilimia 100 na kwamba serikali pia imetenga shilingi bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mbambabay wilayani Nyasa.
“Kwa namna ya pekee tunamshukuru Jemedari wetu Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mikubwa ya bandari katika wilaya ya Nyasa’’,amesisitiza.
Manyanya amesema Serikali inaendelea kuifungua wilaya ya Nyasa katika sekta ya usafiri na usafirishaji hivyo kutoa fursa kwa wawekezaji kufika kuwekeza katika wilaya hiyo yenye fursa nyingi za kiuchumi na uwekezaji.
Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari za Ziwa Nyasa Manga Gassaya, akizungumzia utekelezaji wa ujenzi wa bandari ya Ndumbi, ameitaja miundombinu iliyojengwa katika bandari ya Ndumbi kuwa ni ujenzi wa Gati lenye urefu wa mita 160 kwenda ziwani na sehemu ya kupokea lango la meli yenye urefu wa mita 40.
Miundombinu mingine iliyojengwa katika bandari ya Ndumbi ameitaja kuwa ni ghala la kuhifadhia mizigo lenye mita za ukubwa 1,020,eneo la sakafu ngumu kwa ajili ya kuhifadhia mizigo isiyoathiriwa na mvua lenye mita za ukubwa 9030 na jengo la kupumzikia abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 70,000 kwa mwaka.
Gassaya alisema bandari ya Ndumbi baada ya kukamilika Desemba 2022 imeongeza uwezo wa kuhudumia shehena kwa bandari za ziwa Nyasa kwa mwaka kutoka tani 76,000 hadi kufikia tani 110,000.
Alisema bandari hiyo pia imeongeza uwezo wa kuhudumia abiria kutoka abiria 56,000 kwa mwaka hadi kufikia abiria 126,000.
Meneja huyo wa bandari za ziwa Nyasa amesema serikali pia imeanza kutekeleza ujenzi wa bandari mpya ya kisasa ya Mbambabay lengo likiwa ni kuimarisha ushoroba wa maendeleo ya Mtwara ambayo ni njia fupi na rahisi kuhudumia mizigo ya Malawi kutokea bandari ya Mtwara.
“Serikali ya Awamu ya Sita imetenga shilingi bilioni 70 kuanza kutekeleza mradi huo ambao unatarajia kukamilika ndani ya miezi 24,ujenzi wa bandari ya Mbambabay ukikamilika utaongeza uwezo wa kuhudumia shehena ya mizigo katika bandari kutoka tani 110,000 hadi kufikia tani 550,000 kwa mwaka’’,alisema.
Hata hivyo alisema baada ya ujenzi wa bandari mpya ya Mbambabay kukamilika,makao makuu ya bandari za ziwa Nyasa yatahamia Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma kutoka bandari ya Kiwira iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya.
Alisema kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika bandari za ziwa Nyasa,katika kipindi cha miezi sita ya mwaka 2023/2024 bandari zimehudumia jumla ya abiria 7,358 na mizigo tani 1,828.6.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inasimamia bandari 15 katika ziwa Nyasa zilizopo katika mikoa ya Ruvuma,Mbeya na Njombe.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best