December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Nkasi watakiwa kutumia mradi wa umwagiliaji kujiinua kiuchumi

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Charles Makongoro Nyerere amewataka Wananchi wa Kata za Kipili, Kirando na Itete wilayani Nkasi kutumia fursa ya mradi wa umwagiliaji unaojengwa katika kata hizo kuinua kipato chao.

Huku akiwataka Wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo ili uwe na manufaa kwa jamii kama ilivyokusudiwa na serikali.


Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo wakati akishuhudia utiaji saini na makabidhiano ya mradi wa skimu ya umwagiliaji Lwafi-Katongolo kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Mkandarasi M/S Halem Construction Company Limited.


Amesema licha ya serikali kutumia fedha nyingi kukamilisha mradi huo hautakuwa na maana kama watashindwa kuutunza na kuulinda,lengo ni kuona uzalishaji unapanda,wakulima kulima kilimo cha kibiashara na kujikwanua kiuchumi na jamii inabadilika inakuwa na maisha bora.


Kwa upande wake Mhandisi Lucas Mganda ambaye ni Msimamizi Mkuu wa mradi huo ameeleza kuwa mradi utagharimu bilioni 20.9 na utakelekelezwa kwa siku 720 sawa na miezi 24 ambao utakamilika Julai 25,2026.


Amesema kuwa mradi huo ukikamilika utawanufaisha wakazi 30,000 wa Kata hizo tatu na kuwezesha kumwagilia hekta 33,000 na kuongeza kiwango cha uzalishaji hadi kufikia gunia 50-75 kwa hekta moja .


Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Stephen Kayogolo ameeleza kuwa kati ya miradi iliyokuwa ikijadiliwa kwa upana katika vikao mbalimbali vya Halmashauri ni pamoja na mradi huo licha ya serikali ilikua ikiendelea kutoa fedha kila wakati lakini zilikua hazikidhi ukamilishaji wa mradi huo kwa asilimia 100 .


Ndoto yao ya kuwa na skimu kubwa ya umwagiliaji wilayani Nkasi na Mkoa kwa ujumla imefikiwa ,Wananchi wajipange kuhakikisha mradi huo wanaotumia ipasavyo katika kujiletea maendeleo.


Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kasikazini Aida Khenan ,amewataka viongozi kutoingiza masuala ya kisiasa wakati wa utekelezaji wa mradi huo na kuwaacha Wataalamu wautekeleze mradi huo kiutaalamu.

“Maamuzi ya kisiasa yakiingizwa kwenye utekelezaji wa mradi huo watafika sehemu watakwama na kuuharibu mradi ambao unategemewa kwa kiasi kikubwa na Wananchi wa kata hizo tatu za mwambao wa ziwa Tanganyika,”.


Awali Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nkasi Aljabri Sudi wataendelea kuisumbua serikali kuhakikisha mradi huo unatekelezeka sawa na mkataba waliotiliana na kuwataka Wananchi kuwa walinzi wa mradi huo Kwa kuhakikisha vifaa vyote vya ujenzi haviibiwi.


Kwa upande wao Wananchi wa Tarafa ya Kirando wameeleza kuwa mradi huo ni mkombozi kwao na kuahidi kuwa watakuwa wa kwanza kuulinda na kuhakikisha unakamilika ipasavyo.